Na Shomari Binda, Musoma
Wazazi na Walezi wa watoto wenye ulemavu wametakiwa kuhakikisha wanapelekwa shule na kupata elimu kama walivyo watoto wengine.
Kauli hiyo imetolewa leo Januari 14 na mbunge wa viti maalum mkoa wa Mara, Agnes Marwa, wakati wa ziara yake kwenye shule ya msingi Nyarigamba A iliyopo Manispaa ya Musoma.
Amesema elimu ni haki ya kila mtoto kuipata na serikali ya awamu ya tano inasisitiza kila mtoto kupata elimu stahiki kutokana na uhitaji wake.
Mbunge huyo ambaye yupo kwenye ziara ya kuangalia shughuli za Maendeleo Mkoa wa Mara, amesema wapo wazazi na walezi ambao bado wanawafungia ndani watoto wenye ulemavu.
Akikabidhi fimbo ya kutembelea pamoja na vifaa mbalimbali kwenye shule hiyo, mbunge huyo amesema wapo watoto wenye ulemavu ambao wanafanya vizuri darasani na wengine wanasaidia familia zao.
Kila mtoto anapaswa kupata elimu na wanaoishi na ulemavu ni muhimu kupewa kipaumbele na kutimiza mahitaji yao ikiwemo vifaa vya kutembelea.
“Serikali ya Dk. John Magufuli inataka kula mtoto apate elimu na wanasoma bure sasa kwa nini wengine wafungiwe ndani hatuwezi kukubaliqna na jambo hili,”amesema Agnes.
Kwa upande wao walimu na wanafunzi wa shule ya msingi Nyarigamba A, wamemshukuru mbunge huyo kwa misaada aliyotoa na kuwasaidia wenye ulemavu.
Wamesema ni viongozi wachache wenye moyo wa kusaidia na kusaomba viongozi wengine kuwa na moyo wa kusaidia.