Na Sheila Katikula, Mwanza
Wazazi na walezi katika kata ya Nyamagana iliyopo jijini Mwanza wametakiwa kutambua vipaji vya watoto wao ili waweze kuwaendeleza katika masomo na kutimiza ndoto zao za baadae.
Hayo yalisemwa na Diwani wa Kata ya Nyamagana, Bhiku Kotecha kwenye hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Nyamagana iliyopo jijini hapa ya kuwapongeza walimu kwa matokeo mazuri.
Alisema kuwa lengo la hafla hiyo ni kuwapongeza walimu hao kwa juhudi zao za kuimarisha ufaulu kwa wanafunzi wanaohitimu darasa la Saba mwaka jana.
Kotecha alisema kuwa matokeo mazuri kwa Wanafunzi hutokana na kufanya kazi kwa ushirikiano kati ya walimu na wanafunzi na kujituma.
Aliongeza pia nidhamu nzuri katika maeneo ya kazi ni njia moja wapo ya kuleta Chachu ya maendeleo ya kielimu katika shule husika.
Nimefura hishwa na juhudi zenu katika kazi kwani kutoa mwanafunzi bora wa kwanza siyo mchezo ndiyo manaa nimeatoa mifuko miwili ya sukari yenye ujazo wa Kl 25, jiko la gesi na ngao katika shule ya msingi nyamagana kama zawadi ya kuwapongeza walimu,” alisema Kotecha.
Naye Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Nyamagana, Anadoreen Rugaimukamu alisema kuwa kati ya shule zilizopo kwenye kata 18 wilayani Nyamagana kata ya Nyamagana imekuwa ya kwanza imetoa mwanafunzi bora wa kwanza wa kiume wilayani humo.
Alisema ushindi huo umetokana na ushirikiano mzuri waliokuwa nao kati ya walimu na wazazi katika suala zima la kutambua umuhimu wa masomo pamoja na malezi bora.
Jelly Geogre ni Mwanafunzi aliehitimu darasa la Saba katika Shule ya Msingi Nyamagana mwaka 2020 na alifanikiwa kushika nafasi ya kwanza katika ngazi ya Wilaya.
Alisema siri ya mafanikio ni kuwisikiliza walimu kwa umakini walichofundisha na kujisomea kwa bidii ndiyo imepelekea kufanya vizuri kwenye mtihani huo.
“Niliweka utaratibu wa kujisomea mara kwa mara na mwalimu akinifundisha sijaelewa namfata kwa muda wangu ofisini ili anielekeze tena, malengo yangu ni kuwa Daktari wa moyo kwa sasa nasoma shule ya sekondari Ipwaga iliyopo Misungwi jijini hapa,” alisema George.
Kwa upande wake Baba Mzazi wa Jelly alisema kuwa nidhamu nzuri waliyomfunza tangu akiwa mdogo imesaidia kwa kiasi kikubwa kufanya vizuri kwenye masomo yake.
Afisa Elimu kata ya Nyamagana, Bertha Ntanwa, amewataka walimu kuendelea na utaratibu waliokuwa wakifanya katika kuwatambua wanafunzi wenye vipaji na kuwaendeleza sanjari na kuwahiza Wenye uwezo mudogo kujituma.
“Tumetoa vyeti kama zawadi kwa walimu waliofaulisha vizuri kwenye masomo wanayofundisha nawaomba muendelee kujituma katika kazi ili mwakani tupate watoto wengi waliofanya vizuri,”alisema Ntanwa.