27.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Wazazi timizeni wajibu wenu katika malezi-Mwalimu Maulid

Na Patricia Kimelemeta, Mtanzania Digital

WAZAZI na Walezi wametakiwa kutoa ushirikiano wanapowapeleka watoto kwenye vituo vya kulea watoto (day care) ili pale wanapopata changamoto za kiafya waweze kupatikana na kumuwaisha kwenye kituo cha afya kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mwalimu Abdul Maulid amesema hayo hivi karibuni na kudai kuwa baadhi ya wazazi na walezi wanashindwa kutumia wajibu wao.

Mwalimu Maulidi ambaye pia ni Ofisa Elimu Mkoa huo amesema kuwa, baadhi ya wazazi na walezi wanapompeleka mtoto kwenye kituo hawawafuatilii, badala yake wanambebesha jukumu la malezi mwenye kituo na mwalimu jambo ambalo sio sawa katika malezi ya mtoto.

” Kuna baadhi ya wazazi wanadiriki kubadilisha hadi namba za simu huku jukumu la malezi likiachwa kwa dada mlezi ambaye hana taarifa sahihi za historia ya ugonjwa wa mtoto, jambo ambalo ni hatari kwa afya ya mtoto pindi anapougua kwa sababu atashindwa kupelekwa kwenye kituo cha afya kwa wakati,” amesema Mwalimu Maulid.

Ameongeza kuwa, ikumbukwe kuwa, vituo vya kulea watoto wadogo (DCC) vinachukua watoto wadogo wenye umri kuanzia miaka miwili hadi minne, hivyo basi wazazi na walezi wanapaswa kushirikiana na wamiliki na walimu kila wakati Ili kujua mienendo ya matibabu ya mtoto.

” DCC inachukua watoto wadogo sana ambao hawawezi kujieleza na kwamba wanahitaji uangalizi wa hali ya juu katika malezi yao ili waweze kukua katika hali ya utimilifu, lakini wazazi sasa hivi hawatimizi wajibu wao, wakishampeleka mtoto kituoni basi hata simu haipatikani,” amesema Mwalimu.

Ameongeza kuwa, jukumu la malezi anaachiwa mmiliki wa kituo na mwalimu, huku dada wa nyumbani akilea mtoto anavyopenda yeye bila ya kujali kama mtoto mgonjwa au la, jambo ambalo linahatarisha maisha ya mtoto.

Amesema kuwa, ifike wakati kila mmoja atimize wajibu wake, wazazi washirikiane kwa karibu na wamiliki wa kituo na mwalimu wao ili kufuatilia mienendo ya watoto wao na endapo tatizo litajitokeza inakua rahisi kwao kutafutana na kuangalia namna ya kumsaidia mtoto kabla tatizo hilo halijawa kubwa.

Amesema kuwa, katika kipindi hiki ambacho Serikali inatekeleza Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) kuanzia umri sifuri hadi miaka minane, inawataka wadau wote hadi Asasi za kiraia kushirikiana katika malezi ya mtoto kupitia afua tano za afya, lishe, ulinzi na usalama, elimu na malezi yenye mwitikio.

Mwalimu Maulid amesema kuwa, kwa upande wa Mkoa wa Dar es Salaam, serikali imewapa elimu ya afya walimu wa madarasa ya awali ili kuwatambua watoto wanaougua ghafla na kuwahi kuwapeleka kituo cha afya kupatiwa matibabu huku wakiendelea kuwatafuta wazazi au walezi wao.

” Walimu wa madarasa ya awali wamepewa elimu ya afya ya mtoto ili inapotokea wameugua ghafka waweze kuchukua hatua za haraka ikiwa ni pamoja na kuwapeleka kwenye vituo vya afya kupatiwa matibabu pamoja na kuwapa huduma ya kwanza huku wakiendelea kuwatafuta wazazi au walezi.

” Tumewapa elimu ya afya walimu wote wa madrasa ya awali ili inapotokea mtoto maeugua ghafka hawaishwe kituo cha afya kupatiwa matibabu pamoja na kupewa huduma ya kwanza, ndiyo mana Kila shule Ina ‘ first Aid Kit’,” amesema.

Ameongeza kuwa, lengo la serikali kujenga shule karibu na vituo vya afya ni pamoja na kurahisisha shughuli za matibabu kwa watoto.

Naye mmiliki wa kituo cha kulea watoto cha Saba Junior kilichopo Manispaa ya Ubungo, Zakaria Kisanga amesema kuwa, wazazi na walezi hawatoi ushirikiano pindi mtoto anapougua ghafla na ukiwatafuta simu walizoandika kituoni hazipatikani.

” Kuna mtoto aliugua ghafla kwenye kituo chetu, tulipompigia simu mzazi namba haipatikani, tukalazimika kumtafuta dada mlezi ambaye alituambia tumrudishe nyumbani mpaka mzazi wake atakaporudi kwa sababu hana historia ya matibabu ya mtoto, jambo ambalo tuliona linaweza kuhatarisha afya ya mtoto, tukalazimika kumpeleka kituo cha afya kwanza ili apatiwe matibabu huku tukiendelea kufanya Mawasiliano nao,” amesema Kisanga.

Aliwataka wazazi na walezi hao kuhakikisha kuwa, wanapowapeleka watoto wao kwenye vituo hivyo wanapaswa kufuatilia ili kujua hali ya afya zao na kutoa namba ambayo itapatikana Kila wakati Ili inapotokea tatizo iwe rahisi kiwasiliana nao, jambo ambalo linaweza kusaidia malezi ya mtoto.

Hata hivyo, baadhi ya wazazi wamesema kuwa, kitendo cha kuwapeleka watoto kwenye vituo bila ya kufuatilia Malezi yake kunaweza kuhatarisha maisha ya mtoto.

” Sisi wazazi wa miaka ya hivi karibuni hatuwajibi kabisa, tumeshindwa kuwalea watoto wetu badala yake tunaenda kuwabwaga kwenye vituo ili walelewe na walimu, kitu ambacho ni tofauti na miaka ya zamani,”amesema Othman Ally mkazi wa Dar es Salaam.

Ameongeza kuwa, serikali inapaswa kuweka sheria kali ya kuwabana wazazi wanaoshindwa kuwajibika kwa watoto wao katika malezi wachukuliwe hatua za kisheria, jambo ambalo litakua fundisho kwa wengine.

Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoani humo, Nyamara Elisha amesema kuwa, mtoto anapougua anahitaji kufarijiwa na kubembelezwa, kitendo cha mzazi kutokuwepo kunaweza kumsababishia msongo wa mawazo au kuzidiwa.

“Mtoto akiugua anahitaji faraja ya mzazi huku anabembelezwa, ikiwa mzazi hatokuwepo kunaweza kumsababishia kuzidiwa na kuhatarisha maisha yake,” amesema Nyamara.

Ameongeza kuwa, ifike wakati wazazi watimize wajibu wao, wanapowapeleka watoto kituoni wanapaswa kufuatilia na kujua maendeleo yao na pale inapogundulika kuwa mgonjwa anapaswa kushiriki kikamilifu kumpeleka kituo cha afya kupatiwa matibabu na kubembelezwa na sio kumwachia mlezi au dada wa kazi abebe majukumu ya mzazi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Bright Jamii Initiative (BJI), Irene Fugara aliwataka wazazi kutoa ushirikiano kwenye malezi ya mtoto kwa sababu utasaidia kuondoka changamoto zinazojitokeza.

“PJT- MMMAM inataka Malezi Jumuishi ya mtoto kuanzia umri sifuri hadi miaka minane, hivyo basi kila mmoja kuanzia mzazi, jamii, wadau hadi Serikali tunapaswa kushirikiana ili kuhakikiaha mtoto anakua katika hali ya utimilifu,” amesema Fugara.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na serikali mwaka jana, zinaonyesha kuwa, vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua kutoka 147 kwa vizazi hai 1000 kwenye utafiti wa TDHS ya mwaka 1999 hadi kufikia vifo 43 vya watoto hai 1,000 kwenye utafiti wa TDHS-MIS ya mwaka 2022.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles