Na Renatha Kipaka, Bukoba
WAZAZI na Walezi mkoani Kagera wametakiwa kutumia unga wa soya kwa kuchanganya kwenye chakula cha mtoto mdogo kwani unasaidia kumpa lishe bora mtoto kutokana na unga huo kuwa na protini nyingi.
Ushauri huo umetolewa juzi na Katibu wa Kikundi cha maendeleo ya wanawake kilichopo Manispaa ya Bukoba kijulikanacho kama Bukoba Women Empowerment Assiciation (BUWEA) kinachojihusisha na utengenezaji wa maziwa ya soya Apolina Beda wakati akizungumza na Mtanzania Digital ambapo amewashauri wazazi na walezi kutumia unga wa soya ili kujenga afya za watoto wao.
“Ktokana na Mkoa wa Kagera kuwa na kiwango cha udumavu kwa watoto kikundi chetu kilikuja na suruhisho la kuanzisha kiwanda cha kutengeneza maziwa ya soya na kusindika unga lengo likiwa ni kujenga afya bora kwa watoto kwa kuhamasisha wazazi na walezi.
“Mtoto chini ya miaka nane anapotumia unga wa soya unamsaidia kumjenga kimwili na kiakili hivyo kumsaidia kupata kinga kutougua maradhi ya mara ikiwamo kumsaidia kukua akiwa na afya njema,” amesema Beda.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikundi hicho, Regina Majaliwa, ameeleza kuwa, kikundi hicho ni mwavuli wa vikundi 138 vyenye jumla ya wanachama 1,280 ambavyo vinajishughulisha na ujasiliamali, kilimo, ufugaji na uzalishaji wa maziwa ya soya na unga wa soya.
Majaliwa ameongeza kuwa kiwanda chao kinazalisha maziwa ya soya kati ya lita 200 hadi 300 kwa mwezi kutokana na watu wanaohitaji, lakini mashine zina uwezo wa kuzalisha lita 100 hadi 200 kwa siku hivyo ameomba jamii mkoani humo na maeneo ya jirani kutumia bidhaa yao kwani ni dawa tiba kwa watoto na kwa watu wa rika zote wakiwemo wazee.
Ikumbukwe kuwa mkoa wa Kagera unakabiriwa na kiwango cha udumavu asilimia 37 kwa mwaka 2020/2021.