Na TIMOTHY ITEMBE -TARIME
WAWINDAJI haramu 570 wamekamatwa kwa kipindi cha miezi sita mwaka 2016 katika Hifadhi ya Serengeti wakifanya shughuli za uwindaji wa wanyamapori kinyume cha sheria.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa juzi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), James Mbugi, wakati akikabidhi mradi wa bwawa la maji katika vijiji vya Gibaso na Karagatonga vilivyopo Kata ya Kwihacha, Wilaya ya Tarime mkoani Mara.
Alisema wawindaji hao walikamatwa kuanzia Julai hadi Desemba, mwaka jana ndani ya hifadhi hiyo wakiwinda wanyama pori kinyume cha sheria na tayari wamefikishwa mahakamani.
Akizungumzia mradi huo bwawa la kunyweshea mifugo, Mbugi ambaye pia ni Meneja Ujirani Mwema wa Tanapa, alisema umejengwa kwa nguvu za wananchi kwa kushirikiana na shirika hilo na umegharimu Sh milioni 74. Wananchi wamechangia Sh milioni 18.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kwihacha, Mustapha Masyani, alipongeza Tanapa kwa kuwachimbia bwawa na kuwapunguzia wafugaji adha ya kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji ya kunywesha mifugo yao.
Pia aliwaomba kuwaongeza birika la kunyweshea mifugo kwa sababu lililopo halitoshi kwa kuwa mifugo iliyopo katika kata hiyo ni mingi.
Naye mmoja wa wakazi wa Karagatonga, Lucas Manga (60), alisema bwawa hilo litakuwa msaada mkubwa kwao kwa sababu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kutembea umbali wa kilomita tano hadi Mto Mara kwenda kuchota maji na kunywesha mifugo na kushauri kuundwa kwa kamati ya maji ya kusimamia mradi huo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga, aliwataka wakazi wa vijiji hivyo kuheshimu mradi huo na kuutunza ili udumu na kuwa msaada kwao kwa kipindi kirefu.