Na MALIMA LUBASHA -SERENGETI
WATU wawili wakazi wa Wilaya ya Serengeti mkoani Mara wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuwaua simba wawili katika eneo la Kijiji cha Nyichoka wilayani hapa.
Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu, alisema wanyama hao wanaonekana walikuwa na majeraha ya risasi sehemu mbalimbali za miili yao, huku akieleza kuwa Jeshi la Polisi, Idara ya Wanyamapori wanaendelea na uchunguzi tukio hilo.
“Inadaiwa tukio hili lilitokea baada ya kundi la simba kudaiwa kuvamia zizi la ng’ombe la mkazi mmoja wa kijiji hicho…nimeelezwa kwamba Simba mmoja amepona, upelelezi utakapokamilika Serikali itachukua hatua za kisheria dhidi ya wanaohusika,” alisema Babu.
Babu aliwataka wananchi wanaoishi karibu na hifadhi hiyo kuchukua hadhari mbalimbali kulinda mifugo yao na maisha yao kutokana na kwamba wako jirani na mapori ya akiba.
Mwaka 2015, katika Kijiji cha Parknyigoti, simba saba waliuawa kwa sumu baada ya kuvamia zizi la ng’ombe la mkazi mmoja na kuua ng’ombe wake eneo linalohifadhiwa na Hifadhi ya Wanyamapori Ikona WMA.