29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, December 19, 2024

Contact us: [email protected]

WAUZA UNGA HUTENGENEZA USHAHIDI KUKAMATISHA WASIOHUSIKA

Askari Ufilipino wakiwa wameizunguka maiti ya mtu waliyemuua kwa tuhuma kwamba anahusika na biashara ya dawa za kulevya.

Na Luqman Maloto,

JULAI 25, mwaka jana, saa 5 usiku, kijana wa Kifilipino, Restituto Castro, alipokea ujumbe wa simu kutoka kwa mtu asiyemfahamu, kumtaka aende sehemu inayoitwa MacArthur Highway, Manila.

Alipofika hapo, akakuta kawekewa mtego. Ghafla alijikuta amezungukwa na askari, jirani yake kukawa na kifurushi chenye dawa za kulevya. Castro ni mmoja wa watu wa mwanzo kabisa kuuawa kwa tuhuma za dawa za kulevya.

Saa chache kabla ya Castro kutolewa nyumbani kwa ujumbe wa simu, Rais wa Ufilipino, Rodrigo Duterte alikuwa ametangaza kiyama dhidi ya wauza unga. Alipitisha uamuzi kuwa wauawe mara moja.

Duterte alisema siku hiyo: “Hatutaacha mpaka muuza unga mkubwa wa mwisho na muuza unga mdogo wa mwisho, wajisalimishe ama tuwafunge jela au tuwazike ardhini.”

Kauli hiyo kali, imekuwa ikilaumiwa na wengi kwamba watu wasio na hatia wametengenezewa ushahidi bandia kisha kuuawa, Castro anatajwa kuwa mmoja wa waliouawa bila hatia.

Hili ndilo wingu zito lililotanda Ufilipino, kipindi hiki Rais Duterte ameamua kuua wauza unga. Inabainishwa kuwa wauza unga wenyewe wamejiweka kwenye mikono salama, halafu wale ambao hawajawahi kushughulika kabisa na biashara hiyo, wanatajwa kisha kuuawa.

Castro alikuwa baba mwenye familia yake, akiwa na mke pamoja na watoto wanne. Rekodi za maisha yake zilikuwa safi, aliishi kwa kipato halali na hakuwa mwenye makundi maovu, ila alipowekewa mtego tu, akanasa na kuuawa.

Tatizo kubwa la Ufilipino ni kuwa Duterte amewapa maagizo mazito polisi. Aliwaambia: “Timiza wajibu wako na kama katika mchakato wa kutimiza wajibu wako utaua watu 1,000 nitakulinda.

“Kama unamjua mtumiaji yeyote wa dawa za kulevya nenda kamuue mwenyewe, ukiwaacha wazazi wake waifanye hiyo kazi wataumia sana.”

Kwa kauli hizo za Duterte, Ufilipino imefunguliwa awamu mpya ya mauaji. Polisi wanamtaja na kumuua wanayemtaka kisha ripoti zinatolewa kuwa aliyeuawa ni ama muuza unga au teja.

ORODHA BANDIA

Duterte anayo majina milioni moja ya watuhumiwa wa dawa za kulevya. Mmoja baada ya mwingine wanaendelea kuuawa kutoka kwenye orodha hiyo. Inaelezwa kuwa wauza unga pia wameichezea hiyo orodha.

Alvin Manalac, kijana wa Ufilipino, amenukuliwa na gazeti la The New York Times, toleo la Januari 10, mwaka huu akisema alikuwa mtu salama na mwenye kujiamini kwa sababu hahusiki na biashara ya dawa za kulevya.

Manalac anasema katikati ya Oktoba, mwaka jana, alifuatwa na polisi na kumpa taarifa kuwa jina lake naye limo kwenye orodha ya wauza unga.

“Nilishtuka, mimi nimekuwa mpambanaji dhidi ya vitendo vya uhalifu, kuna watu nimesidia wamekamatwa kwa sababu kwa namna moja au nyingine ni wauza unga, sasa na mimi  nimetajwa,” alisema Manalac.

Anaongeza: “Nimeshirikiana sana na polisi kubaini na kukamata wahalifu. Kipindi Duterte akiwa meya wa Manila, yaani kabla hajawa rais, mimi nilishiriki kwenye vita yake ya kupambana na wauza dawa za kulevya.

“Baada ya kujitoa kila upande kumsaidia Duterte dhidi ya uhalifu, nami najikuta nimetajwa kwamba nimo. Ndiyo hapa napata wasiwasi, je, kuna atakayesalimika? Maana hata sisi wengine ambao ni safi, tunachukuliwa tayari ni wahalifu wa kuuza dawa za kulevya.”

Kimsingi hivyo ndivyo wauza unga huharibu mpambano dhidi yao. Wakati wowote vita inapotangazwa, wao hutumia fedha nyingi kuhakikisha hawamulikwi, zaidi hutengeneza ushahidi wenye kuumiza wengine.

Wakati Ufilipino kuna ambao wanauawa kwa sababu ya tamko la Duterte, Marekani kuna wengine wapo jela, wengine wakiwa wamesota muda mrefu baada ya awali kutengenezwa mpaka kumridhisha jaji kwa ushahidi uliopo, hivyo kutoa hukumu kali dhidi yao.

Ndiyo maana vita dhidi ya dawa za kulevya inataka anayechunguza naye achunguzwe. Watu wenye kuendesha mapambano dhidi ya dawa za kulevya, hutakiwa kuchunguzwa kama wanafanya kazi sawasawa kwa ukweli na uaminifu.

Ni kama ambavyo wauza unga wanavyochunguzana wao kwa wao. Siku hata siku hufuatiliana kuona nani hufanya mawasiliano na polisi au kuwa karibu na mamlaka za Serikali.

Sababu ni uwepo wa mapandikizi (snitches). Serikali kupitia mamlaka za kupambana na dawa za kulevya, hupenyeza wapelelezi wao ndani ya mitandao ya wauza unga ili kupata taarifa zote kamili na kuzifanyia kazi.

Wauza unga pia hupenyeza watu wao serikalini hususan kwenye mamlaka za udhibiti wa dawa za kulevya, hivyo kuwa wanapata kila kitu kutoka serikalini. Taarifa hizo huzitumia kuizidi ujanja Serikali na kuendelea kufanya biashara hiyo haramu kwa kujiachia.

Siri moja kubwa ya wauza unga kufanikiwa duniani kote ni kuwashika baadhi ya watu muhimu kwenye mamlaka za nchi. Hilo linawezekana kwa sababu kwenye dawa za kulevya kuna fedha nyingi mno.

Unakuta genge moja la wauza dawa za kulevya lina fedha zenye kutosha kuendesha Serikali moja ya Ulaya, acha Afrika. Watu hao wanashindwa vipi kuwa mabosi wa viongozi serikalini? Ndiyo maana mfumo ni kuchunguzana.

Watu wenye nguvu hizo, wanashindwaje kuwatengenezea ushahidi watu wasiohusika ili wakamatwe?

IMETOKEA MAREKANI     

Yolanda Madden ni mama wa watoto wawili, Marekani, alifungwa miaka mitano jela kimakosa. Sababu ni taarifa za uongo zilizotolewa na wauza unga na polisi nao wakamkamata na akahukumiwa kifungo jela.

Barry Cooper, askari wa zamani wa kikosi cha Swat, aliye na rekodi ya kukamata watuhumiwa wa unga mpaka 100 kwa mwaka, wakiwa na ushahidi, baada ya kuacha kazi, aliamua kufundisha jamii jinsi vita ya dawa ya kulevya inavyotakiwa kuendeshwa.

Cooper ameshatoa mfululizo wa DVD zinazoitwa Never Get Busted Again, akieleza kuwa ugumu wa vita hiyo ni kwa sababu askari wengi wanaojua vita ya dawa za kulevya nao wanahusika, wasiohusika hawajui nyayo za wauza unga.

Kupitia DVD ya Never Get Busted Again toleo la kwanza, Cooper alieleza kuwa watu wengi wamekuwa wakituhumiwa na kufungwa jela bila makosa kwa sababu ya taarifa za uongo kutoka kwa wauza unga, lengo likiwa kuwapiga chenga polisi wasifikie magenge yao.

Mfano mmojawapo ambao Cooper aliueleza ni wa Yolanda Madden kuwa alifungwa kimakosa. Kufuatia maelezo hayo, uchunguzi ulifanyika na kufanikisha kumweka huru mwanamke huyo.

Mwanamke mwingine alitajwa na kuvamiwa nyumbani usiku akiwa na mwanaye mwenye umri wa miaka mitatu. Mwanamke huyo alihukumiwa kifungo jela, hivyo akafungwa na mtoto wake wa kike. Hata hivyo, baadaye alionekana alisingiziwa.

Jaji wa Mhakama Kuu Marekani, Jim Gray anasema ndani ya documentary ya How to Make Money Selling Drug kuwa watu wengi wanatengenezewa kesi na kuhukumiwa.

Alisema kuwa watuhumiwa wengi wa biashara ya dawa za kulevya wanakamatwa na kuachiwa kwa sababu ya kukosekana kwa ushahidi ama ni kwa makusudi au bahati mbaya.

Bobby Carlton ni muuza unga aliyekuwa anatengeneza dola 50,000, Sh112 milioni kwa siku. Anasema dawa za kulevya zina mtandao mpana na huwezi kuwajua kwa wingi wao mpaka na wewe uwemo kwenye mzunguko.

Hivyo, kwa maneno ya Carlton, maana yake majina mengi ya nje siyo kweli, maana wauza unga wanajuana wenyewe. Polisi na raia wema hawajui chochote kuhusu wauza unga.

Kwa kigezo hicho, wauza unga nao huamua kuyumbisha dola ili wasikamatwe kwa kutaja wasiohusika. Muuza unga huwa hamtaji mwenzake kwa imani kwamba akikamatwa na kubanwa sasa anaweza kumtaja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles