Na Yohana Paul, Geita
WAMILIKI wa malori wanaofanya biashara ya mchanga na kokoto mjini Geita, mkoani hapa wameiomba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kusitisha kwa muda agizo linalowataka kuanza kutoa risiti za kielektroniki (EFD).
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Fred Chacha, amesema biashara yao inafanyika kwa misimu na haina mwendelezo hivyo wengi wao hawatamudu kutoa risiti za EFD kama walivyoagizwa.
Chacha amesema agizo hilo lina muda wa wiki moja hadi sasa lakini kwa kipindi chote wamekuwa wakilipa tozo, kodi na mirabaha ya serikali bila kukiuka kanuni za biashara na muongozo huo mpya huenda ukaathiri biashara yao.
“Mpaka sasa tumeshindwa kuendesha shughuli kama ilivyokuwa kawaida, ndio maana kama mnavyoona tumepaki magari, shida kubwa ni hayo maelekezo tuliyopewa kwamba tunapaswa kuwa na mashine za EFD,” amesema Chacha.
Meneja wa TRA Mkoa wa Geita, Hasheem Ngoda amekiri kupokea malalamiko hayo na kuahidi kukutana na viongozi wa wafanyabiashara hao na kuafikiana jinsi ya kuendesha biashara hiyo bila kukiuka taratibu na kanuni za kodi zilizopo kisheria.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 36 cha sheria ya usimamizi wa kodi, kila mfanyabiashara anapaswa kutumia risiti anaponunua bidhaa zake, kwa maana nyingine hakuna mfanyabiashara ambaye amesamehewa kutotumia risiti anapofanya biashara.
“Na nyie ni sehemu ya wafanyabiashara, kwa hiyo hamujasamehewa kutumia risiti, na risiti hizi zipo za aina mbili, risiti za mkono za stakabadhi na risiti za mashine za kielektroniki ambazo ndio mnapaswa kutoa,” amefafanua Ngoda.