26.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

WATUMISHI WASIOWASILISHA VYETI KUFUKUZWA KAZI

Na MAREGESI PAUL – DODOMA

SERIKALI imesema ifikapo Machi mosi mwaka huu, watumishi wa umma ambao watakuwa hawajawasilisha nakala ya vyeti vyao vya kitaaluma, watafukuzwa kazi.

Taarifa hiyo imetolewa juzi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki, alipokuwa akihitimisha mjadala wa taarifa ya shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa mwaka 2016/17.

Waziri Kairuki alisema Serikali ya awamu ya tano kupitia wizara hiyo imepanga watumishi wote wa umma wawe na sifa za taaluma zao wanazofanyia kazi.

 “Serikali inachokifanya kwa sasa kwa wale ambao hawajawasilisha vyeti vyao kwa sababu mbalimbali ikiwamo kutokuwa na vyeti, ili wasionewe au kunyimwa fursa ya kuendelea kuwa watumishi wa umma, waliruhusiwa kupeleka index namba ya shule walizosomea,” alisema Kairuki.

Alisema tangu utaratibu huo uanze Oktoba mwaka jana, wapo watumishi waliopeleka na wengine bado.

“Kwa kutumia hizo index namba, Serikali kwa kushirikiana na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), itaweza kufanya uhakiki kama kweli mtumishi husika anacho cheti halali cha taaluma na alihudhuria masomo yake katika shule husika. Kwa hiyo, ifikapo Machi mosi, mwaka huu, kwa mtumishi yeyote ambaye atakuwa hajawasilisha cheti chake cha taaluma au angalau hiyo index namba, Serikali itamfukuza kazi,” alisema Kairuki.

Alisema baada ya kukamilika kwa utaratibu huo, Serikali itachambua watumishi walio kazini kihalali na wenye vyeti vyote vinavyotakiwa.

“Wale walioghushi na wasiowasilisha, tutatoa tamko juu ya hatua zaidi zitakazochukuliwa, hasa kwa wale waliofanya udanganyifu. Katika suala hili, Serikali imedhamiria kubaki na watumishi wa umma wenye sifa na waliobobea katika taaluma wanazofanyia kazi na siyo wadanganyifu ambao pamoja na kutokuwa na ujuzi wa kazi wanazofanya, pia wanawazibia nafasi za ajira wataalamu wengi walioko mitaani baada ya kukosa ajira,” alisema Waziri Kairuki.

Akizungumzia suala la watumishi hewa, Waziri Kairuki alisema tayari uhakiki wa watumishi hao umekamilika ingawa utaratibu huo utakuwa endelevu ili kudhibiti watendaji wasio waaminifu.

Alisema hadi sasa watumishi 1,595 wa umma waliochangia kuwapo kwa watumishi hewa, wamechukuliwa hatua na kwamba kati yao, 16 wanatoka katika wizara tisa na 1,564 wanatoka katika mamlaka ya Serikali za Mitaa.

Kwa upande wa hoja ya uhakiki wa mali za viongozi wa umma, waziri huyo alibainisha kuwa kupitia matamko yaliyowasilishwa kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, tayari umefanyika uhakiki wa viongozi 116 ingawa kabla ya Juni, mwaka huu, viongozi 500 wanatarajiwa kuhakikiwa mali zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles