23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

WATU 50,000 HUGUNDULIKA NA SARATANI KILA MWAKA

 

 

Na LEONARD MANG’OHA – DAR ES SALAAM

IDADI ya watu 50,000 hugundulika kuwa na ugonjwa wa saratani kila mwaka nchini, huku kati yao 5,000 tu, sawa na asilimia 100 ya wagonjwa wote hufika hospitali kupata matibabu.

Pamoja na idadi hiyo ndogo ya wanaojitokeza kupata matibabu, asilimia 70 hufika hospitalini wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa huo, ambayo ni vigumu kwa mgonjwa kupona.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Saratani Duniani, Mkurugenzi wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Profesa Ayoub Magimba, alisema zaidi ya asilimia 50 ya watu wanaopatwa na saratani wana umri wa miaka kati ya 30 na 59.

“Kundi hili la watu ndio nguvu kazi ya taifa letu. Kwa hiyo tunaona ni kwa namna gani tunapoteza nguvu kazi ya taifa, hivyo ni vema wakati tunaadhimisha Siku ya Saratani Duniani tukaepuka viashiria vya ugonjwa huu, ikiwa ni pamoja na matumizi ya pombe,” alisema Profesa Magimba.

Alisema taarifa ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kwa kipindi cha mwaka 2006 hadi 2015 inaonesha kuwa saratani ya shingo ya kizazi ndiyo inaongoza kwa asilimia 32.8, ikifuatiwa na saratani ya matiti asilimia 12.8, huku ngozi ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na asilimia 11.9.

Saratani ya mfumo wa chakula na njia ya chakula ni asilimia 10.9, kichwa na shingo (7.5%), matezi (5.4%), damu (4.7%), kibofu cha mkojo (3.0%), macho (2.6%) na saratani ya tezi dume (2.1%).

Alisema kwa wanaume saratani ya ngozi inaongoza kwa kuwa na asilimia 24, saratani ya koo (16%), tezi dume (10%) na saratani ya matezi (9%).

Kwa upande wa wanawake, saratani inayoongoza ni ya mlango wa kizazi kwa asilimia 44, ngozi (15%), matiti (14%) na saratani ya koo (5%).

Profesa Magimba alisema tafiti zinaeleza kuwa ikiwa hatua madhubuti za kinga, uchunguzi na tiba stahiki hazitachukuliwa haraka, tatizo la saratani litaongezeka na kufikia wagonjwa wapya milioni 24 duniani kote ifikapo mwaka 2035, huku ongezeko kubwa likitarajiwa katika nchi zinazoendelea, ikiwamo Tanzania.

Alivitaja vyanzo vya ugonjwa huo kuwa ni pamoja na maambukizi yanayotokana na virusi vinavyosababisha saratani ya tumbo, bakteria wa saratani ya tumbo na parasaiti ambao ni vimelea vinavyosababisha saratani ya kibofu.

Vyanzo vingine ni mtindo wa maisha, ikiwamo unywaji pombe kupita kiasi, uvutaji sigara, kula mlo usiofaa kama vile vyakula vyenye mafuta mengi, kutokula matunda na mbogamboga za kutosha matumizi ya dawa za kulevya na kutofanya mazoezi.

Vingine ni mionzi inayotokana na miale ya jua ambayo huwaathiri zaidi watu wenye ulemavu wa ngozi, urithi kutoka kwenye familia, hasa kwa saratani ya matiti na utumbo, pamoja na vyanzo vingine visivyojulikana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles