Renatha Kipaka, Muleba
Watumishi wapya wa kazi za mkataba kada ya udereva na ukusanyaji wa mapato, wamesaini mikataba na kupewa mafunzo yatakayowawezesha kutimiza majukumu yao.
Akizungumza katika hafla hiyo ya utiaji saini wa mikataba pamoja na mafunzo kwa waajiriwa hao, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, Magongo Justus amewaeleza kuwa kazi zinahitaji uaminifu na jitihada binafsi.
Amesema endapo hawatakuwa waaminifu na wenye bidii maana yake hawataweza kufanya kazi kwa ufanisi na wakishindwa kufanya kazi kwa ufanisi itakuwa ni njia ya wao kuondolewa .
“Niwambie tu mmepata mafunzo baada ya mafunzo mtapangiwa vituo vya kazi na mtapewa malengo, ili kufikia malengo mtakayopangiwa mnahitaji kufanya Kazi zenu kwa bidii maarifa, utii na nidhamu,” ameeleza Magongo
Hata hivyo, amewataka wakusanya mapato kuwaheshimu watu wote watakaokutana nao kwenye vituo vyao vya kazi na kuwambia kuwa kwa kuwaheshimu watu ndio wataweza kufanikiwa katika majukumu yao na wataweza kufika mbali kimafanikio.
“Mwonekano wako uwakilishe Muleba. Heshima inategemea na malezi, mheshimu kila utakayekutana naye. Unapokuwa na heshima inakubeba na ikikubeba itakufikisha unakotaka kwenda. Heshimu kazi yako,” amesema magongo
Aidha, amewasihi waliosaini mikataba ya ukusanyaji wa mapato kuepuka tamaa za kutaka kufanikiwa kwa haraka na hata kutorosha mapato kuwa wakifanya hivyo watakuwa wanaziweka hatarini kazi zao na hiyo itawapelekea kuchukuliwa hatua na kusimamishwa kazi zao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Muleba, Elias Kayandabila amewasihi wakusanya mapato kwenda kutenda haki ili kinachotakiwa kupatikana kwa ajili ya Halmashauri kiweze kupatikana.
Ameongeza kwa kuwaeleza kuwa umewekwa muda wa matazamio wa miezi mitatu ili kubaini kama kweli mtu ni mtiifu na mwaminifu na ndani ya miezi mitatu ni rahisi kuwabaini watumishi wanaofaa na wasiofaa.
Lakini pia amewaambia kuwa kwa watakao kuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia maadili kwa mwaka mzima mkataba waliosaini utakapoisha watakuwa na nafasi kubwa ya kuongezewa muda mwingine.
Naye Mwanasheria wa Halmashauri Wakili Muyengi Muyengi amesema kuwa yeye kama Mwanasheria atahakikisha kila anayekusanya mapato ya Halmashauri anakusanya kwa kuzingatia makubaliano na kwa atakayekiuka Taratibu, Sheria na Kanuni hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.