Na Gurian Adolf-Nkasi
WATUMISHI wanne wa Idara ya Ardhi na Maliasili, Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, wanashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya Sh milioni 1.2 kutoka kwa wafugaji.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Said Mtanda, alisema watumishi hao walikamatwa juzi saa mbili usiku baada ya kunasa kwenye mtego waliowekewa na Takukuru.
Alisema kuwa siku moja kabla ya kukamatwa kwa watumishi hao, walifanya operesheni ya kukamata mifugo ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Mfili na kufanikiwa kukamata ng’ombe 40 waliokuwa wameingia kinyume cha sheria.
Mtanda alisema baada ya kukamatwa kwa ng’ombe hao, wafugaji hao walitozwa faini ya Sh 350,000 papo hapo, huku wakitaka fedha nyingine wazilipe kwa njia ya mtandao wa simu kwa kuwa hakuwa na fedha nyingine mkononi.
Alisema baada ya ofisi yake kupata taarifa hizo, ikaweka mtego kwa kushirikiana na Takukuru na kufanikiwa kukamatwa fedha hizo zilizotumwa kwa njia ya M-pesa
“Maofisa hao walifanya kitendo hicho kinyume cha sheria ambapo walipokea fedha hizo bila kutoa stakabadhi kwa mujibu wa sheria. Na hizi fedha tulifanikiwa kuzikamata baada ya kutumwa kwa mke wa mmoja wa watumishi hao ambapo naye anahojiwa na Takukuru kwa hatua zaidi,” alisema Mtanda.
Aliwataja watumishi hao kuwa ni Nicodemus Hillu, ambaye ni Ofisa Ardhi na Maliasili, askari wa wanyamapori Sylivesta Soneka, Justin Makandi, Anselimo Godian pamoja na mke wa mmoja wa maofisa hao aliyemtaja kwa jina la Rahel Nkumbo.