NAIROBI, KENYA
WATUMIAJI wa simu nchini Kenya huenda wakatozwa ada zaidi katika ununuzi wa muda wa maongezi na huduma ya mtandao.
Hii ni baada ya serikali kutangaza mpango wa kuongeza kodi ya ongezeko la thamani(VAT) kutoka asilimia 10 hadi 15.
Nyongeza hiyo, imejumuishwa katika pendekezo la Rais Uhuru Kenyatta kwa Bunge kufuatia tamko lake la wiki iliyopita.
Pendekezo la tozo hilo jipya la kodi likiidhinishwa na Bunge litazidi kuwaumiza watumiaji wa simu, ambao tayari wanakabiliwa na gharama ya ongezeko la ada ya huduma za kutuma fedha.
Serikali iliongeza ushuru unaotozwa huduma hiyo kwa asilimia 10 Julai mwaka huu ili kuwezesha kupatikana fedha za kugharimia mpango wa bima ya afya kwa wote ifikapo mwaka 2022.
Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini Kenya, ushuru huo utaathiri watumiaji wa simu zaidi ya milioni 44.1.
Serikali imekuwa ikihamasisha Wakenya kuzingatia malipo ya kielektroniki ili kuboresha huduma na kupunguza visa vya udanganyifu.
Huduma ya kutuma na kupokea fedha kwa njia ya simu, M-Pesa ilikuwa kwa asilimia 14.2, ambayo ni sawa na Sh bilioni 62.9 za Kenya kwa mwaka wa fedha ulioishia Machi 2018.
Kodi mpya inayowalenga watumiaji wa simu za mkononi imetokana na ukosoaji mkali dhidi ya serikali kupinga mpango wake wa awali wa kuongeza kodi ya bidhaa za mafuta kwa asilimia 16.
Hoja hii ilizua malalamiko makubwa ya umma hatua, ambayo ilimfanya Rais Kenyatta kuingilia kati suala hilo kwa kuipunguza hadi asilimia 10.
Rais Kenyatta amesema kuwa bado kuna pengo katika bajeti ya serikali na ndio sababu ya kupendekeza hatua hizo za kufunga mkanda na kubana matumizi katika idara zote za serikali
Mapendekezo hayo, hata hivyo yanatarajiwa kujadiliwa bungeni jana.