27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

Watu watatu wakamatwa kwa kukutwa na nyara za Serikali Simiyu

Na Samwel Mwanga,Simiyu

JESHI la polisi Mkoa wa Simiyu limefanikiwa kukamata watu watatu kwa tuhuma ya kukutwa na Nyara za serikalI ambazo ni wanyamapori Swala wapatao 28 aina ya Thomson wakiwa wameuawa.

Afisa Mhifadhi wa Pori la Akiba Maswa mkoani Simiyu, Lawrence Okode akizungumza na Waandishi wa Habari jinsi wanyama Swala wapatao 28 aina ya Thomson walivyouawa na majangili.

Watuhumwa waliokamatwa ni Masunga Madede(58), Musa Masinga (28) na Yunis Makwaya(45) wote wakazi wa Kijiji cha Mwasilimbi Wilaya ya Bariadi mkoani humo.

Kamanda wa polisi mkoani Simiyu, Kamishina Msaidizi wa polisi (ACP), Edith Swebe akizungumza leo Agosti 18, na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Bariadi amesema kuwa Agosti 17, mwaka huu katika kijiji hicho walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao wakiwa na swala hao pamoja na pikipiki aina ya King Lion yenye namba za usajili T. 874 CUA ndani ya nyumba ya Musa Masunga

Kamanda Swebe amesema jeshi hilo kwa kushirikiana na Jeshi la Uhifadhi waliofanya operesheni ya pamoja katika kijiji hicho na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao.

“Jeshi la polisi mkoa wa Simiyu kwa kushirikiana na Jeshi la Uhifadhi tulifanya operesheni ya pamoja katika kijiji cha Mwasilimbi katika kata ya Ihusi iliyopo tarafa ya Nkololo wilaya ya Bariadi na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao watatu.

“Watuhumiwa hao walikutwa na nyara za Serikali ambazo ni wanyamapori swala 28 aina ya Thomson wakiwa wameuawa pamoja na pikipiki aina ya King Lion ndani ya nyumba ya Musa Masinga,” amesema.

Kamanda Swebe amesema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa watuhumiwa hao wamekuwa wakijihusisha na biashara hiyo ya nyara za serikali ambapo uchunguzi unaendelea kwa kushirikiana na askari wanyama pori ili kubaini mtandao wao.

Ameendelea kueleza kuwa watuhumiwa hao pamoja na vielelezo walivyokamatwa navyo watafikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria.

Aidha, Jeshi la polisi mkoa wa Simiyu linatoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kuwinda wanyamapori bila kufuata Sheria, Kanuni na taratibu zilizowekwa na pia wamewaomba wananchi kutoa taarifa za majangili ili tuweze kulinda raslimali zetu kwa manufaa ya kizazi cha kesho.

Naye, Afisa Mhifadhi wa pori la Akiba la Maswa mkoani humo, Lawrence Okode amesema kuwa kwa wanyama hao kuuawa kumeisababishia Serikali hasara ya Sh milioni 38 sambamba na kuwapoteza wanyama hao ambao wanalindwa kisheria.

Amesema wataendelea na operesheni hiyo ya kuwakamata watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo vya kijangili na watu wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Operesheni kali inaendelea katika maeneo yaliyo kandokando ya pori la Akiba la Maswa ilikubaini wanaofanya biashara hizo haramu, hivyo natoa wito kwa wanaojihusisha na biashara hizo kuacha mara moja na hatutomfunbia macho mtu yeyote anayejihusisha na biashara haramu ya ujangili,”amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles