Na Nyemo Malecela, Kagera
ATUHUMIWA sita kutoka kisiwa cha Bumbire kijiji cha Iroba, mwalo wa Mahaiga wamekamatwa wakijishughulisha na uvuvi haramu katika doria iliyoendeshwa na Mtendaji wa Kata, Mtendaji wa Kijiji, Afisa Uvuvi wa kata kwa kushirikiana na kikosi kazi cha operesheni cha wilaya dhidi ya uvuvi haramu.
Katika msako huo watuhumiwa hao walikutwa na samaki wadogo chini ya kiwango cha sentimita aroibaini na nane kinachostahili kuvuliwa aina ya Sangara na nyavu haramu aina ya timba vipande 15 kila kipande kina urefu wa mita mia moja.
Baada ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao, Mkuu wa wilaya ya Muleba, Toba Nguvila ameagiza watuhumiwa hao kufikishwa mara moja mahakamani na kusomewa mashtaka ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
“Wilaya ya Muleba bado ipo kwenye operesheni ya kupambana na kuondoa uvuvi haramu. Tulipata taarifa juzi usiku kutoka kwa watoa taarifa wetu na kuagiza kikosi kazi kwa kushirikiana na watendaji wa eneo husika kwenda kufanya doria ndipo walifanikiwa kuwakamata vijana hawa.
Wamekamatwa wakivua samaki walio chini ya viwango wengine hawafiki hata robo kilo. Huu ni uharibifu usiovumilika na tutaendelea kuwakamata na kuwachukulia hatua mpaka watakapoacha kujihusisha na uvuvi haramu,” alisema Nguvila.
Alisema kama samaki hao wangeachwa na kuvuliwa wakiwa na viwango vinavyostahili wangeongeza pato kwa taifa na kutoa onyo kwa matajiri wanaowafadhili wavuvi hao na kuacha kazi hiyo na kwenda kutafuta kazi nyingine kwani kazi hiyo haiwezi kuwalipa na kusisitiza kuwa wakikamatwa watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Pia ametoa onyo kwa wataalamu wa uvuvi kutoshiriki katika uvuvi haramu na kuwataka wawe waaminifu na wazalendo wanapotekeleza majukumu yao.
Kwa upande wake Afisa Uvuvi wa kijiji cha Iroba, Bamanya Deogratias alisema kuwa doria ya kuwakamata wavuvi hao ilifanyika kwa ushirikiano wa maafisa uvuvi pamoja na watendaji wa kata na kufanikisha kukamata mitumbwi mitatu iliyokuwa na wavuvi sita na kukutwa na samaki waliochini ya kiwango na timba vipande 15 zenye jumla ya urefu wa mita1500 zenye thamani ya shilingi milioni mbili.
Naye Afisa Uvuvi wa Wilaya, Wilfred Tibendelana alieleza kuwa aina ya nyavu za timba zilizokamatwa zina rangi sawa na maji hivyo samaki akiwa anatafuta chakula akiingia kwenye nyavu hizo hawezi kutoka, matokeo yake kwa siku moja nyavu hizo zinaweza kufanya uharibifu wa tani moja na nusu.
Watuhumiwa tayari wamefikishwa mahakamani kwa ajili ya kuendelea na hatua zingine za kisheria.