TAFITI za hivi karibuni zinaonesha kuimarika kwa afya za wanadamu duniani kote, wakiishi miaka mingi zaidi kuliko ilivyokuwa awali.
Hata katika mataifa masikini duniani ikiwamo Tanzania kiwango cha umri wa kuishi kimepanda kwa wastani wa miaka 10 tangu mwaka 1980.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Serikali nchini, wastani wa umri wa kuishi kwa wanawake ni miaka 63 ambao ni mkubwa zaidi ukilinganisha na wanaume ambao ni miaka 60.
Umri huo umepanda kutoka miaka 50, wastani uliokuwa katika miaka ya 1980, matokeo ambayo yameelezwa kutokana na ukuaji wa uchumi na kupungua kwa umasikini wa kipato sambamba na kuimarika kwa huduma za afya.
Kwa wastani wa dunia, wanaume sasa kwa wastani wanategemea kuishi hadi miaka 69 wakati wanawake wanafikisha wastani wa miaka 75 kuishi.
Lakini pia wastani wa umri, ambao watu wanaishi wakiwa na afya njema nayo inakua.
Pamoja na habari hizo njema, hata hivyo, ongezeko hilo kwa watu kuishi wakiwa na afya ni la miaka sita tu, ikimaanisha kwamba watu huishi miaka mingi wakiwa na ugonjwa au ulemavu uliotokana na maradhi au kuzeeka.
Wataalamu wanaamini kuwa hilo linatokana na anguko kubwa la kiwango cha vifo vinavyotokana na maradhi mengi ya kuambukiza ikiwamo VVU/Ukimwi, malaria na kipindu pindu.
Kiwango cha watu wanaofariki dunia kutokana na maradhi ya moyo na mishipa ya damu na saratani pia kimeanguka – lakini kwa kasi ndogo, hii ni kwa mujibu wa gunduzi za kitafiti.
Lakini pia maradhi yasiyo ya kuambukiza, ambayo yanatokana na staili za maisha kama vile moyo, kiharusi na kisukari yanasababisha vifo saba kati ya 10 kwa mujibu ya watafiti.
Christopher Murray, Mkurugenzi wa Taasisi ya Afya na Tathimini katika Chuo Kikuu cha Washington nchini Marekani, ambacho kiliongoza utafiti huo, anasema matokeo ya utafiti yanatoa picha ya mafanikio yasiyo sawia ya hali ya afya duniani, yakichagizwa na maendeleo ya uchumi.
“Kukua kwa maendeleo katika taifa au eneo, hata hivyo hakumaanishi kuwa kutakuwa na afya njema,” anasema katika taarifa yake kuhusu matokeo ya utafiti huo uliochapishwa na Jarida la Utabibu la The Lancet.
“Tunaona nchi ambazo zimeboresha maisha zaidi zinaweza kuelezwa kwa kipato, elimu au uwezo wa kushika mimba.
“Pia tunaendelea kuona nchi, ikiwamo Marekani, ambazo zina tatizo la masuala ya afya licha ya utajiri wao mkubwa.”
Pamoja na wastani wa umri wa kuishi, utafiti huo ulioenda kwa jina la Mzigo wa Maradhi Duniani, ulichambua sababu 249 za vifo, maradhi 315 na vihatarishi 79 katika mataifa na maeneo 195 kati ya mwaka 1990 na 2015.
Utafiti huo unahesabika kama kazi kubwa zaidi ya kimamlaka duniani kuhusu visababishi vya maradhi na vifo vya mapema duniani.
Utafiti ulionesha visababishi muhimu vya afya duni, ulemavu na vifo kwa nchi moja moja.
Pia ilikadiria wastani wa maisha ya afya, idadi ya miaka watu wanayotegemea kuishi wakiwa na afya njema na ule wakiwa na maradhi au ulemavu.
Ilibaini kwamba wakati wastani wa maisha ya afya uliongezeka katika nchi 191 kati ya 195 –kwa miaka 6.1 kati ya mwaka 1990 na 2015, haikupanda kwa wastani mzuri wa maisha, ikimaanisha watu wanaoishi miaka mingi zaidi wakiwa na ugonjwa na au ulemavu.
Miongoni mwa maeneo tajiri duniani kama vile Bara la Amerika ya Kaskazini kulikuwa na wastani mbaya wa maisha yenye afya wakati wa uzazi kwa wanaume na wanawake.
Kisukari, ambacho mara nyingi kinahusishwa na watu wenye uzito mkubwa na au wanene, na matumizi mabaya ya dawa ikiwamo mihadarati, husababisha kiwango kikubwa cha afya mbovu na vifo vya mapema nchini Marekani; ilibainisha.
Ilisema kuwa kuna maendeleo katika upunguzaji wa maji yasiyo salama, lakini mlo, unene na matumizi ya mihadarati yanaendelea kuwa tishio.
Wanawake zaidi ya 275,000 walikufa kutokana na matatizo ya mimba au wakati wa kujifungua mwaka 2015, wengi wao ikitokana na sababu ambazo zinaweza kuzuilika.
Vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano vilipungua kwa kiwango cha nusu tangu mwaka 1990, lakini kumekuwa na maendeleo ya taratibu katika kupunguza vifo vya watoto wachanga.
Ilibaini pia maumivu ya kichwa, matatizo ya meno na upotevu wa usikivu na uoni ukimkabili mtu zaidi ya mmoja kati ya 10 duniani.