Watalii saba kutoka Korea Kusini wamefariki dunia katika ajali ya boti iliyotokea kwenye mto Danube katika mji mkuu wa Hungary, Budapest.
Watalii wengine 21 bado hawajulikani waliko. Boti ya kitalii iliyokuwa ikiwabeba ilipinduka na kuzama karibu na jengo la bunge la Hungary baada ya kugongana na boti nyingine kubwa zaidi wakati mvua ikinyesha majira ya saa tatu na dakika 15 usiku wa kuamkia leo.
Ubalozi wa Korea Kusini mjini Budapest umesema jumla ya watalii 33 walikuwa ndani ya boti hiyo.
Msemaji wa huduma za uokozi nchini Hungary Pal Gyorfi amesema watu saba walionusurika ajali hiyo wamepelekwa hospitali wakiwa katika hali nzuri.
Polisi wamefanya kazi usiku kucha kujaribu kutafuta wale wasiojulikana walipo, lakini matumaini ya kuwapata wakiwa hai yamefifia. Ubalozi wa Korea Kusini umesema watalii hao hawakuwa wamevaa vesti za kuwasaidia kuelea.