Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
ZAIDI ya watu milioni 2.8 ambao sawa na asilimia 85 wamepatiwa chanjo ya ugonjwa wa uviko 19 katika Mkoa wa Dar es salaam tangu ilipozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hasani, Agosti 30, mwaka Jana.
Akizungumza kwenye warsha ya majadiliano iliyoandaliwa na Internews kuhusu umuhimu wa Chanjo hiyo katika jamii Afisa Afya Mkoani hapa Enezael Ayo, amesema watu wamehamasika kutokana na elimu pamoja ongezeko la vituo vya uchanjaji.
Amesema Kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2012, mkoa wa Dar es salaam ulikuwa na makadirio ya idadi ya watu Milioni 6, ambapo malengo ya uchanjaji yakiwa ni kuwafikia idadi ya watu milioni 3.3
“Tunaendelea kuhamasisha wananchi waendelee kuchanja kwani chanjo ni salama na Haina madhara Kwa binadamu kama uvumi unavyoelezwa huko mitaani.
“Tegemeo la rasilimali ya nchi Ni watu hivyo Basi hakuna kiongozi wa nchi anayependa watu wake kufariki Kwa sababu ndio rasilimali ya taifa,” amesema Ayo.
Amesema mkoa huu ulilazimika kuongeza vituo maeneo mbalimbali Kwa ajili ya uchanjaji ambapo awali vilikuwa vituo vitatu tu mpaka sasa Kuna vituo 318.
Kwa upande wake, Daktari anayejitegemea, Dk. Christina Mdingi, amesema jamii inatakiwa kupuuza baadhi ya viongozi wa dini mbalimbali wanao eneza uvumi kuwa Chanjo hiyo si salama sababu hakuna taarifa ya madhara yatokanayo na uchanjaji.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC), Samson Kamalamo, amesema mafunzo haya yatasaidia Wanahabari kutoa taarifa sahihi Kwa jamii kuhusiana na ugonjwa huo.
“Yote tuliyojifunza hapa tunaenda kuyafanyia kazi, Kwa sababu huu ni mwanzo tu tumejiandaa kufanya mikutano mingine pamoja na warsha Kwa lengo la kuwafanya wananchi kuwa aware,” anasema Kamalamo