KINSHASA, DRC
MAPIGANO ya ukabila yaliyotokea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wiki iliyopita yamesababisha zaidi ya watu 500 kukimbilia Uganda.
Wakimbizi hao wamewafahamisha maofisa wa Uganda na Shirika la Umoja Mataifa linalowahudumia Wakimbizi (UNHCR) kuwa mapigano hayo kati ya jamii za Lendu na Bagerere yamelitumbukiza eneo la mashariki mwa Congo katika hali ya sintofahamu.
Makundi hayo ya wakimbizi kutoka jimbo la Ituri mashariki mwa nchi, yanafanya safari za hatari kuvuka Ziwa Albert lililoko mpakani mwa nchi hizo mbili wakitumia mitumbwi isiyo na ubora.
Wengi wao ambao ni wanawake na watoto, wameshuhudiwa wakiwa na mizigo yao hususan magodoro.
Kinachowatia hofu na wasiwasi viongozi wa wilaya za Hoima na Kikuube ni uwezekano wa kuzorota hali ya usalama.
Inahofiwa huenda kuna uwezekano wa wakimbizi kuingia Uganda wakiwa wamejihami kwa silaha.
Shaka nyingine ambayo wimbi hilo jipya la wakimbizi kutoka DRC ni namna watu hao wanavyowasili bila kupitia njia rasmi za mipakani ambako wangepimwa kabla ya kutangamana na jamii za Uganda.
Wakazi wana wasiwasi kuwa kuna uwezekano wa milipuko ya magonjwa ya Ebola na kipindupindu.