24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kauli ya IGP Siro kwa trafiki isimamiwe vizuri

TUMEPATA kuandika mara nyingine na leo tunarudia kwamba askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani (trafiki), wanahitaji kuwa na elimu ya ziada ili kuondokana na kasumba ya kuwaandikia madereva adhabu ambazo hazina mbele wala nyuma.

Jambo hili limekuwa likizungumzwa na viongozi wa ngazi za juu, lakini utekelezaji umekuwa hafifu mno na mwisho wa siku mwananchi wa kawaida ndiye anayeumia.

Si kwamba tunaunga mkono madereva wasiandikiwe au kupigwa faini kulingana na makosa wanayotenda, lakini yapo makosa ambayo hayana msingi kwa trafiki kumwandikia faini ya Sh 30,000, pengine palikuwa panahitajika maelekezo tu kwa mhusika.

Mwenendo huu umekuwa kero kubwa kwa watumiaji wa barabara ambao wamefikia hatua ya kuwaita trafiki “TRA” yaani Mamlaka ya Mapato Tanzania, badala ya kutoa elimu.

Leo tunasema haya, baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro kutoa tena maekelezo ya aina hii juzi kwa trafiki kutimiza majukumu yake pasipo kumwonea mtu.

Akionekana kutofurahishwa na mwenendo wa askari hao, IGP Sirro alisema umefika wakati kwa trafiki kutumia busara kabla ya kuchukua uamuzi wa kuandika faini kwani wakati mwingine dereva akipewa maelekezo anakuwa balozi mzuri wa usalama barabarani.

Alisema trafiki anayekuwa kinara wa kuandika faini hizo kwa madereva, leo yuko jeshini na kesho atakuwa raia wa kawaida mitaani ambako atakutana nao, lakini jambo kubwa ni kushauri na kusamehe pale ambako kunastahili.

Hii ni kauli nzito kutolewa na IGP ambayo tunaamini sasa itafungua ukurasa mpya kwa askari hawa ambao gari likisimama mbele yao ni kukimbilia kuingiza namba za usajili kuona kana inadaiwa au laa. Inatia aibu eti hata kama rangi ya gari imepauka unaambiwa ni kosa. Huu ni unyanyasaji mkubwa ambao unapaswa kukemewa vikali.

Kwa maneno ya IGP Sirro, kwanini trafiki wetu hawafikii hatua ya kutoa elimu kwanza, wanakimbilia kuandika faini?

Tunadhani mwenye dawa ya kukomesha unyanyasi wa aina hii bado ni IGP mwenyewe kwa sababu ndiye bosi wao.

Tunakubaliana na IGP Sirro kuwa si kila kosa ni la kuandika faini, inawezekana mtu mwingine haelewi, lakini anapaswa kuelekezwa tu ili asirudie makosa hayo.

Tunasema umefika wakati sasa wa kubadilika.

Ndiyo maana tunasema darasa hili kwa trafiki wetu linapaswa kusimamiwa kweli kweli ili kuondokana na karaha za aina hii. Siku zote wapo wachache ambao ndio wamekuwa vinara wa kusababisha Jeshi la Polisi kupakwa matope.

Sisi MTANZANIA tunasisitiza kauli hii ya IGP Sirro kuanzia sasa itekelezwe kwa vitendo na askari wa ngazi za chini ambao ndio watendaji kazi wa kila siku barabarani.

Tunasema mambo mengi yanaweza kwenda kwa ushauri tu na si kwa kila jambo dereva aangukie kwenye mikono ya faini kama alivyosema IGP Sirro kwamba trafiki anayemwandikia mwananchi hati ya malipo bila kuridhiana ni kosa, akitoa mfano kuwa kama mwananchi ana leseni bandia kuna mambo mawili ya kufanya, mosi ni kupeleka mahakamani au kuandikiwa hati ya malipo.

Ni kweli trafiki wetu wamesahau kabisa kutoa miongozi ya elimu ya usalama barabarani? Wameamua kujikita na makusanyo kila kukicha?

Tunakupongeza IGP Sirro kwa maelekezo haya ambayo tunaamini yatafungua ukurasa mpya.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles