Tiganya Vincent- Tabora
SIKU chache baada ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kutangaza uwepo wa mgonjwa mmoja wa corona mkoani Tabora, uongozi wa mkoa huo umesema umebaini kuwa mgonjwa huyo alikutana na watu 40 na 33 wamepatikana na kuwekwa karantini.
Pia watu wengine saba waliokutana na mgonjwa huyo wanasakwa na kwamba lengo ni kuwapata watu wote ambao walikaribiana naye ili wawekwe karantini kwa siku 14.
Katika hahatua nyingine, mkoa huo umeanza kuweka vipima joto kwenye Stendi Kuu na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kitete ili kudhibiti virusi vya corona.
Lengo la kuweka vifaa hivyo ni kujua hali ya joto la watu wanaokwenda kupata huduma katika maeneo hayo na inapobainika kuwa baadhi yao wana joto la juu, waweze kutengwa na kuchukuliwa vipimo kwa hatua zaidi.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Tawala Msaidizi Mkoa (Afya) Dk. Honoratha Rutatinisibwa, wakati akitoa elimu dhidi ya ugonjwa huo kwa wakazi wa Tabora kwa njia ya redio za kijamii.
Alisema sanjari na hilo kila halmashauri za wilaya mkoani humo zimeanza kununua vipima joto kwa ajili ya kuweka maeneo ambayo yanatumiwa na watu wengi kutoa huduma na kupokea huduma.
Dk. Honoratha alisema Halamashauri ya Wilaya ya Kaliua imeshanunua thermos scanner saba, Urambo tatu, Nzega Mji mbilina Halmashauri nyingine tano zimeshaagiza na zinasubiri.
Aliwatahadharisha wapiga debe katika stendi za magari kutopenda kuwakimbilia kwa wingi kufuata abiria pindi magari yanapowasili kutoka maeneo mbalimbali.
Alisema vitendo vya aina hiyo vinaweza kuwasababisha kupata maambukizi ya virusi vya corona na wakati mwingine kuambukizana.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri alitoa wito kwa watu ambao walikuwa karibu na mgonjwa huyo kujitokeza kwa ajili ya kulinda afya zao na ndugu zao.
Alisema kuendelea kujificha wanaweza kuhatarisha maisha yao na wengine.
Aidha Mwanri amewataka wamiliki wa magari ya abiria kuhakikisha wanapokea wasafiri wahakikishe wameandika taarifa zao sahihi ikiwemo jina kamili, mahali anapoishi, anapokwenda na namba yake ya simu.
Alisema lengo la taarifa hizo ni kutaka kuwepo na urahisi ufuatiliaji endapo kutatokea tatizo la maambukizi ya virusi vya corona.
Aidha aliwataka wasafiri wanaowasili mkoani Tabora kutoka maeneo ambayo yana maambukizi mengi kuhakikisha wanazingatia maagizo ya wataalamu ili waweze kulinda uhai wao na wengine kwa kutoa taarifa sahihi.
Hadi hivi Mkoa wa Tabora una mgonjwa mmoja ambaye yuko katika Wilaya ya Urambo ambapo uongozi wa Mkoa umeongeza nguvu katika utoaji wa elimu kwa kutumia redio za kijamii.