JOSEPH HIZA NA MTANDAO
Ripoti ya pamoja ya mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa (UN) imefichua hali mbaya iliyopo katika shule nyingi duniani na kukumbushia hatari wanazokabiliwa nazo watoto kutokana na uzembe au ukosefu wa utashi wa serikali nyingi.
Pamoja na mambo mengine, ripoti hiyo inasema karibu nusu ya shule zote zilizopo duniani zinakabiliwa na ukosefu wa maji safi ya kunywa, vyoo na vifaa vya kuoshea mikono.
Ripoti hiyo inatokana na utafiti wa pamoja uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, karibu watoto milioni 900 wanakabiliwa na uhaba wa vifaa vya msingi vya usafi wanapokuwa shuleni.
Hilo linamaanisha kwamba maisha ya mamilioni ya watoto yanawekwa katika hatari duniani na hilo linaweza kuwa funzo muhimu juu ya sababu, ambayo watoto huamua kutoenda shule badala ya kuhudhuria na kuugua.
Hilo linakuja licha ya kwamba viongozi wa dunia wametoa ahadi za kutoa maji safi na vifaa vya usafi kwa ajili ya wote na kuhakikisha kila mtoto anapata elimu bora kufikia mwaka 2030 chini ya malengo endelevu ya Umoja wa Mataifa (UN).
Uhaba wa maji salama na vifaa vya usafi kunaweza kusababisha ukosefu wa maji mwilini, maradhi na hata vifo.
Lakini watoto wengi wanalazimika kuhatarisha afya zao ili kwenda shule, kwa mujibu wa ripoti hiyo ya kwanza kumulika huduma zinazotolewa shuleni.
Ripoti imegundua kwamba karibu theluthi moja ya shule za msingi na sekondari hazikuwa na huduma ya maji safi ya kunywa na ya uhakika, na kuathiri karibu watoto milioni 570.
Karibu asilimia 20 ya shule hazina maji safi ya kunywa kabisa.
Zaidi ya theluthi moja ya shule zinakosa vyoo hivyo, watoto zaidi ya milioni 620 huathirika.
Shule moja kati ya tano za msingi na moja kati ya nane za sekondari zinachukuliwa kuwa hazina usafi.
Karibu nusu ya shule hizo hazikuwa na vifaa vya kuoshea mikono, ambavyo ni muhimu kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi kuepuka maambukizi na magonjwa.
Nchi za Afrika zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara, Asia Kusini na Mashariki zilionekana kuwa na miundombinu mibovu.
Ripoti inaongeza kuwa karibu nusu, asilimia 47 ya shule hazitoi sabuni kwa watoto.
Watafiti pia waligundua kwamba watoto waliopo katika shule za awali maarufu kama chekechea na shule za msingi wana uwezekano mdogo wa kupata maji safi na vyoo kuliko wale walio katika shule za sekondari.
Ripoti inaonya kwamba hilo litaathiri watoto wadogo katika wakati wao muhumu wa utambuzi na maendeleo ya kimwili na makuzi, ikiongeza kuwa kipindupindu kinachosababishwa na maji machafu na vyoo duni huua watoto chini ya miaka mitano kila baada ya dakika mbili.
Ripoti inaainisha umuhimu wa usafi na vifaa vya usafi shuleni hususani miongoni mwa wasichana, ambao wana uwezekano mkubwa zaidi wa kuhudhuria shule na kuhitimu masomo yao iwapo kuna mazingira mazuri yanayohakikisha usafi wao.
Moja ya malengo ya maendeleo endelevu ya UN ni kwamba watu wanapaswa kupata maji safi ya kunywa ifikapo mwaka 2030.
Hilo linamaanisha kwamba nyumba zote, shule, maeneo ya huduma za afya na mahali pa kazi kunapaswa kuwe na maji safi ya kunywa na vifaa vya usafi.
Wasichana wanaobalehe ndio mara nyingi hulazimika kukosa masomo wanapokuwa katika hedhi shuleni, ambako hakuna miundombinu bora ya usafi.
Aidha, zaidi ya theluthi moja ya wasichana huko Asia Kusini wanakosa masomo wanapokuwa katika hedhi, kwa sababu mara nyingi hawapati huduma ya vyoo na taulo za kike.
Hiyo ni kwa mujibu wa utafiti ulioendeshwa mapema mwaka jana na Shirika la WaterAid na UNICEF.
Ripoti pia inakadiria kuwa mwaka 2016 wasichana milioni 355 walienda shule ambako hawakuweza kuosha mikono yao baada ya kubadili vitaulo.
Thérèse Mahon, Programu Meneja wa WaterAid kwa ukanda wa Asia Kusini alisema: “Kutoa maji safi na huduma za usafi ni muhimu kwa utoaji wa elimu bora kwa wasichana, ili waweze kusimamia hedhi zao salama na kwa heshima wakiwa shule.”
Kwa mujibu wa ripoti hiyo mmoja kati ya wasichana watatu wa Asia Kusini hawaendi shule kila mwezi kwa sababu ya kukosekana faragha na kutoweza kuosha mikono yao baada ya kubadili vitaulo.
Shule zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika zinatofautiana, kwa mfano nchini Guinea, ni asilimia 10 tu ya shule zina maji safi kulinganisha na asilimia 79 nchini Zambia.
Nchini India, asilimia tano ya shule ziliripotiwa watoto huleta maji ya kunywa kutoka nyumbani – shule hizi huhusisha watoto milioni 19.
Hata hivyo, maeneo ya kijijini, ambako kuna uwezekano mdogo wa kupatikana maji shuleni, ni nusu tu ya watoto wana maji safi na salama majumbani kwao.
Kelly Ann Naylor, mkuu wa kitengo cha maji safi na salama kutoka Unicef anasema: “Iwapo tunaamini elimu ni ufunguo wa kumsaidia mtoto kutoka katika umasikini, upatikanaji wa maji safi na salama ni muhimu kuwasaidia kufanikisha ndoto zao za kielimu.
“Kwa kuliacha suala hili ama kutolijali ilhali tukifahamu linahusisha na ustawi na afya ya watoto tusitarajie maendeleo mazuri kielimu.”
Hata hivyo, Naylor alikiri kuna kazi kubwa ya kushawishi mafungu ya kutosha ya bajeti kuelekezwa katika uwekaji wa maji safi na salama katika shule zote.
Benki ya Dunia mwaka jana ilionya nchi zilitakiwa kuongeza matumizi yake hadi kufikia dola bilioni 150 kwa mwaka ili kuwezesha upatikanaji wa maji safi na huduma ya vyoo.
Hali hiyo inaweza kuimarika kwa haraka endapo tu viongozi watalichukulia suala la maji, vyoo na usafi kama kipaumbele na kwamba utashi wa kisiasa utawezesha utoaji wa huduma bora vinginevyo janga linakuja.