29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

WATOA MAONI TOFAUTI HISA ZA VODACOM KUUZWA DSE

Na JUSTIN DAMIAN – Dar es Salaam

HISA za Kampuni ya Vodacom Tanzania zitaanza kuuzwa wiki ijayo katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), huku baadhi ya wadau wa mambo ya fedha wakitoa maoni tofauti kuhusu uwezo wa soko hilo kuhimili hisa hizo.

Vodacom inakuwa kampuni ya kwanza ya simu za mkononi kutii agizo la Serikali la kuweka katika soko la hisa asilimia 25 ya hisa ili zinunuliwe na umma.

Jumla ya hisa milioni 560 za Vodacom zenye thamani ya Sh bilioni 476 zitauzwa kwa Sh 850 kila moja.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili juzi, Ofisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Moremi Marwa, alisema hisa hizo zitaanza kuuzwa wiki ijayo, ingawa hakutaka kusema ni tarehe ngapi hasa.

Lakini taarifa za uhakika ambazo gazeti hili limezipata, zinasema ufunguzi wa toleo la awali la mauzo ya hisa na dhamana kwa umma kwa ajili ya kukusanya mtaji (Initial Public Offer – IPO) ni Machi 9 na yatafungwa Aprili 19.

Hisa hizo zitauzwa rasmi kwa umma kuanzia Mei 16.

Hata hivyo, hatua ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kuidhinishia Kampuni ya Vodacom Tanzania kuendelea na utaratibu utakaoiwezesha kuuza hisa zake DSE imepokewa kwa mtazamo tofauti na wadau mbalimbali.

Profesa Honest Ngowi ambaye ni mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe tawi la Dar es Salaam, aliliambia MTANZANIA Jumapili kuwa ana wasiwasi kama kampuni zilizoingia soko la hisa ikiwamo Vodacom zitaweza kukusanya kiasi cha mtaji walichokusudia.

“Hizi kampuni za simu zinaingia katika soko la hisa kutokana na msukumo wa Serikali. Lengo ni kukusanya mtaji kutoka kwa umma na kinachokuja hapa ni kuwa yanaingia kwa kufuatana, yakilenga kukusanya mitaji kutoka kwa wateja wachache waliopo sokoni,” alisema Profesa Ngowi.

Mchumi huyo nguli alifafanua kuwa kitendo cha kampuni nyingi kuingia kwa wakati mmoja, ikiwamo pia TCCIA Investment Ltd, kunafanya uwezekano wa kukusanya kiasi cha fedha wanachokusudia kuwa mdogo kutokana na wateja kuwa wachache.

“Wateja wa hisa za kampuni ambazo tayari zimeshajisajili kama TBL, CRBD ndio hao hao tunaotarajia wanunue hisa za kampuni hizi mpya. Mimi ninachokiona hapa ni uwezekano mdogo wa kuweza kukusanya kiasi walicholenga, kwa maana wanunuzi watalazimika kugawa fedha walizonazo ili wanunue huku na kule kadiri kila mmoja atakavyoona inamfaa,” alisema.

Profesa Ngowi aliongeza kuwa kwa sasa hali ya kifedha kwa kampuni na hata watu binafsi ambao ni wateja walengwa wa hisa si nzuri na kwamba kwa mtazamo wake, kampuni mpya zinazolenga kukusanya mitaji, ikiwamo Vodacom Tanzania, zimeingia sokoni katika kipindi ambacho si kizuri.

“Ninachokiona hapa ni kuwa hizi kampuni zinaweza kuwa na wakati mgumu wa kukusanya mitaji tofauti na kampuni kama CRDB, NMB na nyingine ambazo kwanza ziliingia katika kipindi kizuri na pili ziliingia moja moja,” alieleza.

Lakini Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Udalali ya Zan Securities Limited katika Soko la DSE, Raphael Masumbuko, alitofautiana na mtazamo wa Profesa Ngowi kwa kusema kuwa anaamini Vodacom itaweza kukusanya kiasi cha mtaji wanacholenga na hata kuvuka.

“Hatujawahi kuona katika soko la hisa kampuni ambayo ni nzuri watu wakashindwa kununua hisa zake kwa sababu ya tatizo la liquidity (ukosefu wa fedha). Kampuni ya simu kama Vodacom ni nzuri ukilinganisha na nyingine zilizopo sokoni, kwa sababu washiriki wake ni kuanzia watu wa hali ya chini hadi wa juu,” alieleza.

Masumbuko alisema haitawezekana kampuni kuingia sokoni kwa kufuatana. “Kampuni ambayo itaingia kwa karibu sana itakuwa ni kama miezi mitatu hivi. Ndani ya kipindi hiki tunahisi kwamba tayari kutakuwa na wadau tunaowaita speculators, ambao watakuwa wameshanunua hisa na kuziuza, watakuwa tayari kununua za kampuni nyingine,” alisema.

Alipoulizwa na gazeti hili kama anadhani kampuni zinazolenga kujisajili DSE katika kipindi hiki kigumu kiuchumi zitaweza kukusanya kiasi wanachokusudia ikiwamo Vodacom Tanzania, Moremi alisema hawezi kuzungumza chochote kwa kuwa ni suala la kubashiri.

“Swali lako ni gumu, kwa vile ni la kubashiri na mimi nisingependa ninukuliwe nikibashiri hivi au vile,” alisema.

Hata hivyo, Moremi alisema kujiorodhesha kwa kampuni mpya ya simu DSE kutasaidia kuongeza wawekezaji katika soko ambalo kwa sasa lina wawekezaji laki tano kupitia kampuni 25 ambazo zimejiorodhesha.

Alisema Vodacom pia itasaidia ukuaji wa soko ambalo kwa sasa ukubwa wake ni Sh trilioni 21.

“Vodacom peke yake wanafanya IPO ya shilingi bilioni 476,” alifafanua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles