24 C
Dar es Salaam
Sunday, May 19, 2024

Contact us: [email protected]

Watoa huduma wapatiwe mafunzo kuwahudumia watu wenye ulemavu

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Serikali imeshauriwa kuendeleza programu za mafunzo kwa watoa huduma wa afya ili wajue masuala ya msingi wanayopasa kuzingatia pindi wanapowahudumia watu wenye ulemavu.

Ushauri huo umetolewa wakati wa kikao kazi baina ya wauguzi na viongozi wa watu wenye ulemavu walipokuwa wakijadili changamoto wanazokutana nazo katika vituo vya afya ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata huduma bora.

Mkurugenzi wa Chama cha Walimu wenye Uziwi (CWUT), Karim Bakari, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi baina ya wauguzi na viongozi wa watu wenye ulemavu.

Kikao hicho ni sehemu ya utekelezwaji wa mradi wa afya jumuishi wenye lengo la kuboresha mazingira na mawasiliano kwa watu wenye ulemavu unaoratibiwa na Chama cha Walimu wenye Uziwi Tanzania (CWUT).

Akizungumza katika kikao hicho Ofisa Muuguzi kutoka Hospitali ya Vijibweni, Rehema Nyachuma, amesema wanakutana na changamoto mbalimbali wakati wa kuwahudumia watu wenye ulemavu hasa viziwi kwani watoa huduma wengi hawana uelewa wa jinsi ya kuwasiliana nao.

“Wanakuja wagonjwa wengi na foleni inakuwa kubwa mnatoa mafundisho na maaelekeo au tunaita namba lakini inawezekana kuna kiziwi hajui kitu gani kinaendelea. Hali hii inasababisha wengi kushindwa kupata huduma kwa wakati…lakini hata kama ukimtambua wakati mwingine unaweza kushindwa kuwasiliana naye,” amesema Rehema.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Wenye Ualbino Tanzania (TAS), Mussa Kabimba, amesema huduma za afya hapa nchini bado hazijawa jumuishi na rafiki kwa watu wenye ulemavu.

Amesema watu wenye ulemavu wanakumbana na changamoto mbalimbali wanapokwenda kupata huduma za afya kama vile majengo mengi kutofikika kirahisi, ukosefu wa wakalimani, uhaba wa vifaa tiba, uzingatiwaji wa masuala ya kiser na kwamba sera ya afya pia imepitwa na wakati.

“Mfano sisi watu wenye ualbino wengi wana viashiria ama tayari wana saratani ya ngozi hivyo, tunahitaji mafuta kinga kwa ajili ya kuboresha afya ya ngozi kuzuia mionzi mikali ya jua na kofia zenye kingo pana, lakini hospitali zinazotoa huduma ya saratani kwa hapa nchini kuna KCMC, Ocean Road na Muhimbili hivyo mtu anayetoka Kigoma kupata huduma hii bado ni changamoto,” amesema Kabimba.

Mwezeshaji katika kikao hicho Wakili Novat Lukwago, ameshauri kuzingatiwa kwa sera, sheria na miongozo inayotoa haki kwa watu wenye ulemavu ili kuhakikisha wanapata huduma bora kama watu wengine.

Awali Mkurugenzi wa CWUT, Karim Bakari, amesema mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2020/21 kwa ufadhili wa Shirika la Foundation for Civil Society (FCS) kwa lengo la kutatua changamoto wanazokutana nazo watu wenye ulemavu pamoja na watoa huduma za afya.

“Kiziwi akienda hospitali anaweza kushindwa kupata huduma stahiki kwa sababu tu mtoa huduma ameshindwa kuwasiliana naye vizuri, pengine anaumwa tumbo lakini akapewa dawa ambayo si sahihi,” amesema Bakari.

Katika kikao hicho washiriki wamependekeza sera ya afya ipitiwe upya, kuwe na dawati maalumu linalohusu masuala ya watu wenye ulemavu wizarani, watoa huduma wapatiwe mafunzo ya lugha ya alama na utekelezwaji wa bima ya afya kwa wote uharakishwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles