Janeth Mushi, Arusha
Shirika la Kimataifa la WaterAid Tanzania, limezindua na kukabidhi miradi miwili ukiwemo wa uboreshaji miundombinu ya maji safi wa mazingira (Back to School Wash) na mradi wa kubadili tabia kwenye masuala ya mazingira na usafi binafsi (HBCC) iliyogharimu Sh Milioni 280.
Shirika hilo kwa kushirikiana na wataalamu mkoani hapa wanatekeleza miradi miwili katika wilaya za Arusha na Arumeru,ambayo inatekelezwa na shirika hilo na kufadhiliwa na FDCO na Unilever.
Akizungumza leo Jumatano Mei 19,2021, Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la WaterAid Tanzania, Anna Mzinga wakati wa uzinduzi na kukabidhi miradi hiyo katika hopsitali ya Rufaa ya Mt. Meru na Shule ya Msingi Mringa, amesema bado elimu inahitajika juu ya umuhimu wa unawaji wa mikono ili kuweza kujikinga na magonjwa ya milipuko.
Amesema kupitia mradi wa kampeni ya usafi HBCC uliotekelezwa jiji la Arusha wameweza kusanifu na kuweka miundombinu ya kunawia mikono katika maeneo sita ya wazi ya mikusanyiko ikiwemo Hospitali ya Mt. Meru, masoko na taasisi za afya yaliyomo katika kata mbili.
Kuhusu mradi wa usalama wa afya wa mtoto wamejenga sehemu 11 za kuwania mikono katika shule nane za msingi ambazo ni Oldonyosambu, Leminyor, Lemanyata, Selian, Lemanyata, Olosiva, Enaboishu na Mringa zilizopo katika Kata tano zilizopo wilayani Arumeru.
“Chimbuko la miradi hii miwili ni kuwepo kwa ugonjwa wa Covid-19, ambapo katika jitihada za kupambana na athari zake kwa kushirikiana na wadau wetu wa maendeleo tumefanikiwa kutekeleza miradi hii miwili Arusha iliyogharimu Sh milioni 280,”ameongeza Mzinga.
Mkurugenzi huyo amesema katika mradi wa “Back to School” umeweza kunufaisha wanafunzi zaidi ya 5,800 waliowezeshwa miundombinu ya kunawa mikono katika kuzuia na kudhibiti magonjwa ya milipuko huku katika mradi wa HBCC ukiwafikia wananchi zaidi ya 21,000.
“Katika Shule hii ya Mringa imekuwa tofauti na maeneo mengine ambapo miradi hii imechangia nguvu katika jitihada za mpango maalumu wa uboreshaji wa huduma ya afya ya mtoto wa kike kwa kukamilisha jingo maalum la sitara kwa wasichana kwa mahitaji maalum wakatiwa katika hedhi,” amesema Mzinga.
Mbali na Mkoa wa Arusha maeneo mengine ambayo mradi wa ‘Back to School’ unatekelezwa ni pamoja na Zanzibar, Dar es Salaam na Geita, ambapo wamelenga hasa maeneo yenye miji mikubwa kwa kuangalia maeneo ambayo athari ya magonjwa ya milipuko ingeweza kuwa kubwa.
Naye, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mt. Meru, Kipapi Mlambo, ameshukuru wadau hao kwa kuwezesha miradi hiyo na kuwa wagonjwa wanaoingia na kutoka hospitalini hapo wanatumia vifaa hivyo.
“Tunashukuru sana kwani hivi sasa watu wameelimika juu ya umuhimu wa kunawa mikono lengo likiwa ni kupunguza na kujilinda juu ya magonjwa ya milipuko,” amesema Malmbo.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Agnery Chitukulo ameshukuru wadau hao kwa utekelezaji wa miradi hiyo na kuwa watashirikiana na halmashauri na viongozi wa ngazi za chini katika kulinda miradi hiyo.
“Nitoe shukrani kwa kutuwekea vifaa hivi,tumepokea kwenye shule zetu,vituo vya huduma vya afya na masoko, ila tunawaomba ikitokea fursa nyingine msitusahau Arusha kwani bado uhitaji ni kubwa tuna shule za Msingi 805 Shule za Sekondari 261 pamoja na vituo vya afya, hospitali na zahanati nyingi,” amesema.
Moja ya wanafunzi wa Shule hiyo ya Mringa, Shifla Benard,anayesoma darasa la sita shuleni hapo,alishukuru wadau hao na kuwa mbali na umuhimu wa mradi wa maji,chumba cha kujisitiri wakiwa katika hedhi kitawasaidia wanafunzi wa kike ambao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali kutokana na mazingira yasiyo rafiki.