Na Malima Lubasha, Serengeti
WANANCHI pamoja na waumini wa dini mbalimbali wilayani Serengeti mkoani Mara wamehimizwa kuliombea Taifa kudumisha umoja, amani na mshikamano sambamba na kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan.
Rai hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mtanda wakati wa hafla ya futari aliyoiandaa kwa kufadhiliwa na Benki ya Azania kwa waumini wa dini ya kiislamu wilayani Serengeti.
Futari hiyoiliongozwa na Mtanda ambaye kwa sasa ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, ilifanyika mjini Mugumu katika ukumbi wa Chuo cha Uuguzi na Ukunga cha Kisare Nyerere ddh na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali,wakuu wa taasisi za umma na binafsi,viongozi wa dini, waumini, viongozi wa Halmashauri, Madiwani na Viongozi wa vyama.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mtanda alisema kwa sasa ambapo maumini wa dini ya kiislamu wanaendelea na mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ni vyema kuliombea Taifa wakati huo huo kudumisha umoja, amani na mshikamano kwani kuendelea kudumisha amani kunafanya uchumi kuimarika na maendeleo kwa wananchi wakiwemo waumini kwenda vizuri na muda wote waendelee kutekeleza maagizo ya Mwenyezi Mungu.
“Tujitahidi kuhakikisha kwalba tunalinda amani kwani kama hakuna amani hata shughuli zinazofanywa na wananchi haziwezi kufanyika vizuri, niwasihi pia wananchi wa Serengeti kuendelea kushirikiana kama mlivyoniunga mkono kwa kipindi chote nilichokuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara,” alisema Mtanda.
Pia aliwaomba Watanzania, viongozi na wadau kutoka mkoa huu kuendelea kusaidia watu wasiokuwa na uwezo, wajane na yatima ikiwa ni njia ya kutekeleza maagizo ya Mwenyezi Mungu .
Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Benki ya Azania Tanzania, Dk. Rhimo Nyansaho, alisema Benki hiyo imeamua kufuturisha wilayani hapa ikiwa ni kuimarisha upendo na kusaidia wasio na uwezo hata kupata chakula cha jioni.
Dk. Nyansaho alimpongeza Mtanda kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa miradi mbalilmbali mkoani Mara na kuwezesha mkoa huo kuimarisha hali ya ulinzi na usalama.
Alisema shughuli za Benki ya Azania ni kufanya kazi za maendeleo kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu kwenye vikundi kuanzia watu watano ambapo wanatoa mikopo bila kubagua dini huku akiwataka waumini wa dini ya kiislamu kwenda kukopa katika benki hiyo na kuwaasa kujiepusha na mikopo kausha damu yenye riba kubwa.
Aliongeza kuwa kwa utafiti uliofanyika inaonyesha kwamba mikopo ya kausha damu inapungua wilayani hapa baada ya benki hiyo kuanzisha vitengo na kubuni mipango mingi kusaidia vikundi vya vijana na wanawake kwa riba ndogo.
Sheikhe wa Wilaya ya Serengeti, Juma Simba alisema kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan jambo kubwa la msingi ni kuzidisha wema mbele ya Mungu kwani wanadamu ni wakosaji na kusisitiza kuwa Mungu anapenda kuombwa, hivyo alitoa wito kwa watu wa dini mbalimbali kurejea kwa muumba kuomba msamaha.
Sheikh Simba aliwahimiza waislamu kuanzisha vikundi na kujiunga na Benki hiyo ya Azania ambapo aliomba kutengeneza kitengo cha ”Kiislamu kibenki” kwani waislamu wana taratibu zao za kifedha benki na kuwashukuru kwa kuanzisha utaratibu huu kutoa futari na kufuturisha waislamu na wadau wa madhehebu mengine na kuomba mpango huu uwe endelevu.