*Aeleza siri ya kuwa na kilimo chenye tija, zana za kisasa
*Mwarobaini wa sukari pia watajwa
Na Faraja Masinde, Mtanzania Digial
Watanzania wamehimizwa kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi zikiwamo za kilimo ambazo zinapatikana nchini Brazili.
Wito huo umebainishwa leo Agosti 31, 2022 na Balozi wa Tanzania nchini Brazili, Profesa Aderadius Kilangi kupitia mkutano ulioandaliwa na Watch Tanzania kwa njia ya Zoom.
Balozi Kilangi ambaye alizungumza moja kw amoja kutoka Brazili, amebainisha matunda ambayo Tanzania inaweza kuyapata kupitia ushirikiano wake na nchi hiyo hususan katika sekta za kilimo, biashara, uwekezaji na mifugo.
Balozi Kilangi ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Vyombo vya habari kwa njia ya Mtandao wa Zoom, kutokea nchini Brazili ambapo alitumia fursa hiyo kueleza matunda ambayo Tanzania inaweza kuyapata kupitia ushirikiano wake na Brazili.
“Miongoni mwa fursa ziliopo Brazili ni kwenye Sekta ya Kilimo hasa cha Maharage ya Soya, Mtama na Mahindi ya Njano, kuna kampuni tumewasiliana nayo kutoka China imekuja Tanzania, imeanza kulima Soya na tunatarajia itaanza kulima Maharage ya Njano na Mtama, kwa hiyo Wakulima wetu Tanzania wanaweza kuanza kulima mazao haya.
“Kwani kampuni hiyo imeishakuja nchini Tanzania na kwa usimamizi wa Wizara ya Kilimo inaendelea na maandalizi ya kulima zao la soya kwa kiwango kikubwa, ikitarajia kulima ekari 100,000.
“Lakini pia wakulima wetu wa Tanzania wanayofuirsa ya kuweza kulima kwa wingi zao la soya na baadaye mtama na mahindi ya njano,” amesema Balozi Kilangi.
Aidha, amebainisha eneo jingine kuwa ni la zana za kilimo ambapo ubalozi ulitembelea kampuni kadhaa za kutengeneza zana za kilimo kwa hatua zote, yaani zana za: kusafisha mashamba; kung´oa visiki; kulima; kupanda; kupalilia; kumwagilia; kuvuna; kupaki.
“Zana za kilimo zinazotengenezwa Brazil kwa ujumla zinasifika kuwa na ubora mkubwa, ubalozi unashauri kufanya ushirikiano wa karibu na kampuni hizo ili ziweze kufika Tanzania na kusaidia kuboresha kilimo.
“Pia, Ubalozi unatoa wito kwa wadau mbalimbali wa kilimo nchini Tanzania kuanzisha ushirikiano na makampuni ya Brazili ili kupata zana bora na Madhubuti,” amesema Balozi Kilangi.
Pia Balozi Kilangi amegusia kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari ambapo amesema kuwa nchi hiyo inafanya vizuri kwa kuwa kinara kwenye uzalishaji wa sukari duniani.
“Ubalozi umefaulu kufanya ziara kwenye mojawapo ya viwanda vikubwa vya kuzalisha sukari cha Uzina Coruripe mnamo Mei 2022, ambacho pia kinamiliki mashamba makubwa sana ya miwa.
“Ulifanikiwa kuwashawishi kuangalia uwezekano wa kuwekeza Tanzania kwa ubia au kwa njia nyingine yeyote, katika kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari, na wahusika walionesha nia na utayari wa kufanya hivyo.
“Hivyo tunatoa wito kwa wadau wa kilimo cha miwa na utengenezaji wa sukari nchini Tanzania kuangalia uwezekano wa kuitumia fursa hii kwa kuanzisha ushirikiano na Brazili katika kukuza kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari kwa kutumia teknolojia ya kisasa,” amesema Balozi Kilangi.