Na RAMADHAN HASSAN-KONDOA
Watanzania wametakiwa kutembelea vituo vya utalii vya mambo ya kale kikiwamo Kituo cha Michoro ya Miambani, kilichopo Kolo, Kondoa, Mkoa wa Dodoma.
Hayo yalielezwa juzi na Mkurugenzi Msaidizi wa Mambo ya Kale, Fabian Kigadye, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea Kituo cha Michoro ya Miambani cha Kolo, Kondoa.
Wizara ya Maliasili na Utalii juzi ilisafirisha wananchi kwenda katika kituo hicho kilichopo Kolo, Kondoa zaidi ya kilomita 200 kutoka mjini Dodoma ambapo wananchi zaidi ya 300 walikwenda kuangalia michoro hiyo.
Wakiwa katika kituo hicho, wananchi hao walitembelea na kujionea michoro katika maeneo matatu ya site namba B 1, site namba B 2 na site namba B 3, juu ya Mlima Kolo.
Akizungumzia michoro hiyo, Mkurugenzi huyo Msaidizi wa Mambo ya Kale, alisema michoro hiyo imechorwa na Watanzania zaidi ya miaka 50,000 iliyopita.
“Tanzania kuna maeneo saba ambayo ni urithi wa dunia likiwamo eneo la michoro ya miamba Kolo, Kondoa.
“Kwa hiyo, nawaomba Watanzania wawe na utaratibu wa kufanya utalii katika maeneo ya utalii ikiwamo utalii wa mambo ya kale, kwani huko watajionea wenyewe jinsi michoro hii na haya mapango yanavyovutia.
“Kwa sasa, Serikali imejipanga kuhakikisha barabara zinazokwenda katika michoro hiyo zinakuwa katika kiwango kizuri ili watalii waweze kufika kwa urahisi,” alisema Kigadye.
Kwa upande wake, Mhifadhi wa kituo hicho, Amos Mgimwa, alisema maandishi yaliyomo katika michoro hiyo yalichorwa kwa kutumia rangi za njano, nyeusi, nyeupe na nyekundu na kwamba michoro hiyo ilichorwa miaka 50,000 iliyopita na Kabila la Wasandawe.