|Bethsheba Wambura na Elizabeth Joachim, Dar es Salaam
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na Shirika la Umeme (Tanesco), Mamlaka ya Maji na Majitaka Mkoa wa Dar es Salaam (Dawasco) na kampuni za simu, imeanzisha operesheni ya kuwasaka wanaohujumu miundombinu ya kampuni hizo.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema operesheni hiyo imeanzishwa baada ya kuwepo kwa matukio kadhaa ya uhalifu kwa kutumia mitandao na uhujumu wa wa miundombinu ya Dawasco na Tanesco.
“Tumeanzisha operesheni hii maalumu ili kukabiliana na wahujumu uchumi kwa njia ya mitandao na kuharibu miundombinu ya kwa kujiunganishia maji na umeme kinyemela ilihali wakijua ni makosa na wanahatarisha afya zao.
“Watu wasio waaminifu wanatumia mafuta ya transfoma kukaangia chipsi ndiyo maana watu wanaumuka, utakuta mtu shavu la kushoto halilingani na la kulia.
“Wanaojijua wamehujumu miundombinu hiyo wajisalimishe kabla operesheni haijawafikia, tukiwakamata tutawatia mbaroni kwa kesi ya kuhujumu uchumi wa nchi,” amesema Mambosasa.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Dawasco, Cypriani Luhemeja, amesema kutokana na uhujumu huo mamlaka hiyo inapoteza asilimia 40 maji yanayozalishwa.
“kwa sasa tunazalisha maji ya kutosha na tunatarajia hadi kufikia mwaka 2020 wananchi wote wa Mkoa wa Dar es Salaam watapata maji ya kutosha,” amesema.