NA LILIAN JUSTICE, MOROGORO
SERIKALI ya Mkoa wa Morogoro, imesema itachukua hatua kali kwa watu watakaokamatwa wakihujumu miundombinu ya Kampuni ya Simu Tanzania (TCCL).
Onyo hilo limetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Stephen Kebwe, alipokuwa akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa huduma za mtandao mpya wa 4G LTE wa kampuni hiyo ya simu.
Dk. Kebwe alisema TTCL imepewa jukumu la kuwaunganisha wananchi popote walipo kwa mawasiliano ya uhakika, hivyo imebeba jukumu la kufanikisha utendaji wa sekta nyingine zote zikiwamo shughuli za ulinzi na usalama wa nchi.
“Ili TTCL waweze kutoa huduma bora kwa wananchi, ni lazima miundombinu ya simu itunzwe badala ya kuhujumiwa.
“Mimi na kamati yangu ya ulinzi na usalama, tunalipa suala hili uzito unaostahili na atakayebainika akiharibu miundombinu ya kampuni hiyo, tutamchukulia hatua za kisheria,” alisema Dk. Kebwe.
Pamoja na hayo, aliitaka kampuni hiyo kutoa huduma kwa gharama nafuu ili kila mwananchi aweze kunufaika, kwani kampuni hiyo ni mali ya umma.
Kwa upande wake, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba, alisema kampuni hiyo imezindua huduma hiyo kwa kutumia teknolojia ya 4G LTE ambayo ina kasi, kwa sababu inataka kutoa huduma za kuridhisha kwa wananchi.
“Lengo la kuzindua huduma hii ni kuwawezesha wananchi kuwasiliana kwa ufanisi na kwa gharama nafuu zaidi na hivyo kufanikisha shughuli za kiuchumi na kijamii na kuwa na chachu ya maendeleo ya Mkoa na Taifa kwa ujumla.
“Kimsingi, TTCL inatekeleza mpango wa biashara wa miaka mitatu unaolenga kuleta huduma mpya katika soko, kuongeza tija na uwajibikaji ili kutoa huduma bora kwa wateja,” alisema Kindamba.