ESTHER MBUSSI NA HERIETH FAUSTINE, DAR ES SALAAM
WASOMI na wachambuzi wa mambo ya siasa wameipongeza Marekani kwa kufanya uchaguzi huru na wa haki uliompatia ushindi mgombea wa Chama cha Republican, Donald Trump.
Wakizungumza na MTANZANIA, wachambuzi hao wamesema uchaguzi huo uendelee kuwa funzo kwa viongozi wa Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Mchambuzi wa masuala ya siasa nchini na Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Azaveli Lwaitama alisema ushindi wa Trump unatokana na demokrasia iliyokomaa wa nchi hiyo.
Dk. Lwaitama ambaye hivi sasa ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Joshua Kibira mkoani Kagera, alisema Wamarekani wameamua kumchagua Trump kwa sababu hawapendi kutawaliwa na rais kutoka chama kimoja kwa zaidi ya miaka minane na pia kuchaguliwa mtu wa kumpigia kura.
“Si kwamba Hillary Clinton hakuwa na sera nzuri, isipokuwa hawataki rais aliye madarakani awachagulie mtu, wanataka chama kimoja kikitoka kingine kingie. Hapa Wamarekani wanatuonyesa uaminifu wao kwamba hata mtu akiwa mwendawazimu au ana matatizo gani watamchagua tu.
“Trump ana upungufu wake lakini kilichomrahisishia ni Rais Barrack Obama kumpigia debe mpinzani wake. Wanaamini endapo wangemchagua angeendeleza mambo yake kitu ambacho ni kama busu la kifo na Wamarekani hawataki busu la kifo,” alisema Dk. Lwaitama.
Pamoja na mambo mengine, Dk. Lwaitama aliwataka watu waliokuwa na wasiwasi na Trump wakati wa kampeni kuondoa wasiwasi kwa vile Marekani ni taasisi hivyo Trump lazima atekeleze mambo ya Marekani kama taasisi si mambo yake binafsi.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Abdalah Safari alisema huenda ushindi wa Trump utasaidia kuwaondoa madarakani viongozi wa Afrika wababe na wezi wa kura.
Alisema kila mgombea alikua na malengo binafsi. Trump alikua anapinga viongozi wote wezi wanaokaa madarakani kama masultani ambao aliwataja kwa majina wakati wa kampeni zake kama Yoweri Museven wa Uganda, Paul Kagame wa Rwanda na Robert Mugabe wa Zimbabwe.
“Huenda sasa Marekani akiungana na Muisrael anaweza kutusaidia kupata viongozi wa kweli kama inavyofanyika kwao,” alisema.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijo-Bisimba alisema uchaguzi ulikuwa wa huru na haki ndiyo maana Clinton alipoona hakushinda alimpongeza Trump ingawa ameshinda kwa kura chache.
“Ingawa kampeni zake zilikuwa za ubaguzi na aliwasema vibaya waislamu, akawaponda Waafrika kwamba wanachukua kazi za Wamarekani lakini liko jambo zuri walilofanya ambalo hata kama wanaibiana kura basi wanaibiana kwa akili siyo kama huku kwetu watu hadi wananyanga’ana masanduku ya kura mkononi,” alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu), Profesa Gaudence Mpangala alisema matarajio ya wengi yalikuwa ni Clinton akiwamo yeye mwenyewe kwa sababu kwa mara ya kwanza angepatikana rais mwanamke.
“Pamoja na usawa wa demokrasia ya sasa, angepita kwa sababu ya sera zake ambazo niliona ni nzuri kuliko Trump ambaye zake zilikuwa za ubaguzi.
“Marekani ni taifa kubwa, wakati mwingine wanapenda kumchagua mtu wa aina hiyo kuonyesha tofauti,” alisema.
Kwa upande wake Chadema, kimewapongeza wananchi wa Marekani kwa kufanya uchaguzi wao kwa njia ya amani na kukamilisha kampeni za kumpata kiongozi mpya wa nchi hiyo.