MAHAKAMA Kuu Kanda ya Mwanza imekubali maombi yaliyowasilishwa na wapiga kura wanne wa Bunda Mjini dhidi ya Mbunge wa Jimbo hilo, Ester Bulaya, Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Wapiga kura hao kupitia kwa mawakili wao, Costantine Mutalemwa na Yasin Memba, waliiomba mahakama kuwaongezea muda wa kuwasilisha maombi yao baada ya muda wao wa awali wa siku 14 kupita.
Pia waliomba ruhusa ya kuwasilisha rufaa katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.
Akitoa uamuzi huo jana, Jaji Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Joaquine De-Mello, alisema mahakama hiyo imekubaliana na maombi yaliyowasilishwa na wapiga kura hao ya kuomba kuongezewa muda.
Pia ilikubaliana maombi ya kibali cha kuwasilisha maombi ya rufaa katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania dhidi ya uamuzi wa shauri namba moja la mwaka 2015 la kupinga matokeo ya uchaguzi jimbo la Bunda Mjini uliotolewa na Jaji wa Mahakama hiyo, Mohameid Gwae.
“Mahakama imekubali maombi namba 38 ya mwaka 2016 yaliyowasilishwa na wapiga kura wanne wa Jimbo la Bunda kupitia kwa mawakili wao Yasin Memba na Costantine Mutalewa.
“Baada ya kupitia hoja za zote ziliozotolewa na mawakili pamoja na uamuzi wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania katika kesi ya Gobless Lema kuhusu haki ya mpiga kura kufungua shauri mahakamani.
“Mahakama imebaini kuwa tafsiri ya haki ya wapiga kura iliyotolewa na katika kesi ya Lema na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania tafsiri yake haipo wazi hivyo imewaruhusu kuwasilisha maombi yao ya rufaa dhidi ya uamuzi uliotolewa na Jaji Gwae mahakama hiyo iweze kutoa tafsiri sahihi kuhusu haki ya mpiga kura,” alisema Jaji De-mello.
Akizungumza nje ya Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza baada ya uamuzi huo kutolewa, Wakili wa wapiga kura hao, Yasin Memba, alisema amefurahishwa na uamuzi huo wa mahakama na anakwenda kuandaa maombi ya rufaa aweze kuyawasilisha katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.