Na TIMOTHY ITEMBE-TARIME
WASICHANA 300 kati ya 5,000 waliokadiriwa kukeketwa mwaka 2016 wilayani Tarime mkoani Mara, wameokolewa na Kituo cha Ushirika wa Kutokomeza Ukeketaji (ATFGM), kilichopo Kijiji cha Masanga chini ya Kanisa Katoliki.
Akizungumza jana Mkurugenzi Mtendaji wa ATFGM, Sisita Stelle Mgaya, alisema kuwa wasichana 300 wameokolewa kukeketwa ikiwa ni pamoja na kupatiwa elimu juu ya madhara ya ndoa za utotoni pamoja na kupinga unyanyasaji wa kijinsia.
Alisema katika kuhakikisha wanatokomeza vitendo vya ukeketaji, wamekuwa wakisafirisha ngariba kwenda sehemu mbalimbali kujifunza ujasiriamali ili kuwapatia kazi mbadala waachane na ukeketaji.
“Kituo chetu cha Masanga kimejitahidi kuwasafirisha Ngariba 50 kwa nyakati tofauti kwenda kujifunza masuala ya ujasiriamali Kibondo, huku na Sh milioni 150 zikiwa zimetumika lakini bado kuna tatizo la ukeketaji,” alisema Mgaya.
Aidha, Mgaya aliongeza kuwa kazi yao ni kutoa elimu kwa wasichana na wavulana pamoja na wazee wa kimila, mangariba ili kuondokana na mila hiyo potofu yenye madhara kwa jamii.
Kwa upande wake, Ofisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Tarime Vijijini, Victor Kabuje, alisema kuwa licha ya Serikali pamoja na mashirika mbalimbali kutumia gharama kubwa kutoa elimu juu ya madhara ya ukeketaji, lakini bado umeshika kasi wilayani humo.