Na BRIGHITER MASAKI – DAR ES SALAAM
WASICHANA 150 wamepatiwa mafunzo ya kufanya biashara kupitia mitandao ya kijamii, itakayowasaidia kujiinua kiuchumi na kuepukana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto ambao umekuwa ni changamoto kubwa nchini.
Akizungumza na MTANZANIA jana Dar es Salaam, wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo, Ofisa Mawasiliano wa Shirika la Her Initiative, Dayana Aggrey, alisema kuwa mafunzo hayo wanayatoa kwa wasichana kwa kuwa msichana ukijiinua kiuchumi hakuna hatakayeweza kumnyanyasa.
Dayana alisema Her Initiative inahusika na kutoa mafunzo kwa wasichana mbalimbali ili kujikimu na kujiinua kiuchumi ili kuepukana na ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.
“Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa mmoja kati ya wanawake watatu duniani amekutana na ukatili wa kimwili au kingono katika kipindi chake cha maisha.
“Nchini Tanzania takribani wanawake wanne kati ya 10 wamepitia ukatili wa kimwili na asilimia 17 wamepitia ukatili wa kingono katika maisha yao.
“Utafiti uliofanywa juu ya ukatili dhidi ya watoto mwaka 2011 unaonyesha kuwa takribani mvulana mmoja kati ya saba amekutana na ukatili wa kingono kabla ya kutimiza miaka 18, na kati yao asilimia 71 wamekutana na ukatili wa kimwili.
“Hata hivyo, utafiti huo unaonyesha kuwa kwa upande wa watoto wa kike, idadi ipo juu zaidi kwani msichana mmoja kati ya watatu amekutana na ukatili wa kingono kabla ya kutimiza umri wa miaka 18 na asilimia 72 wamekutana na ukatili wa kimwili,” alisema Dayana.
Alisema lengo kuu ni kuwafanya wasichana kujikwamua kiuchumi na kujitengenezea kipato chao wao wenyewe kitakachowasaidia kujikimu kupitia mradi wa Songambele ambao unawasaidia wasichana 18-12 wafanyabiashara walioathirika kiuchumi wakati wa janga la corona.
Pia aliongeza kuwa wasichana hao waliwapata kupitia mitandao na hivyo wanawapa mafunzo na baadae watawafuatilia maendeleo yao watakayopata baada ya mafunzo na kutatua changamoto zao wanazopitia katika biashara zao.
“Tunawapa mafunzo na kuwashauri kuweza kusajili biashara za TRA iliziweze kutambulika,” alisema Dayana.
Kwa upande wake, mwalimu wa mafunzo hayo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Serengeti Biet inayohusika na kusaidia wasichana, Kennedy Mmari alisema kuwa wameyatoa kwa wasichana ili waweze kujua jinsi ya kufanya masoko mtandaoni ili kuepukana na ukatili wa kijinsia.
“Msichana akiinuka kiuchumi anachangia kuleta maendeleo katika ngazi ya familia na taifa. Msichana anapokuwa hana chanzo cha kipato anakuwa muhanga mkubwa wa kukandamizwa na kufanyiwa ukatili wa kijinsia, ndiyo sababu ya kuwapa mafunzo wasichana na wanawake wajasiriamali.
“Tumewafundisha jinsi gani wanaweza kutumia mitandao ya kijamii kufanya biashara na kutofautisha akaunti za biashara na za kwao binafsi, kutafuta wateja kwa njia ya mtandao na kuuza bidhaa zao,” alisema Mmari.