Na FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM
WAKAZI watatu wa Dar es Salaam wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala wakikabiliwa na shtaka la unyang’anyi wa kutumia silaha na kujipatia dola za Marekani 11,800 mali ya Lixue Jiang, raia wa China.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa watuhumiwa hao ambao ni Rajab Imam (20), Hashimu Mussa (25) na Rajabu Hemed (20), kabla na baada ya kufanya hivyo walimjeruhi mlalamikaji kwa kumkata mkono wa kushoto.
Akisoma shtaka hilo jana mbele ya Hakimu Mkazi, John Msafiri, Wakili wa Serikali, Neema Moshi, alisema mahakamani hapo kuwa watuhumiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo Desemba 20, mwaka jana maeneo ya Kariakoo, Dar es Salaam.
Alidai kuwa watuhumiwa kabla na baada ya kupora fedha hizo walimjeruhi kwa kumkata na panga mlalamikaji kwenye mkono wake wa kushoto jambo ambalo ni kosa na kinyume cha sheria.
“Watuhumiwa mnakabiliwa na shtaka la unyang’anyi wa kutumia silaha na mlijipatia fedha dola za Marekani 11,800 mali ya Jiang… kabla na baada ya kutekeleza unyang’anyi huo mlimjeruhi mlalamikaji kwa kumkata na panga kwenye mkono wake wa kushoto,” alidai Wakili Neema.
Hata hivyo, watuhumiwa walikana shtaka hilo na kurejeshwa rumande hadi Januari 17, mwaka huu kutokana na shtaka lao kutokuwa na dhamana kisheria.