Na Mwandishi Wetu,
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango ameipongeza Mamlaka ya Soko la Mitaji na Dhamana (CMSA) kwa juhudi zake za kutoa elimu na kuwazawadia  wanaofanya vizuri katika sekta ya mitaji nchini.
Alikuwa akizungumza katika hafla ya kutoa zawadi na kuwapongeza wanafunzi wa vyuo vikuu walioshinda shindano  kuhusu masoko ya mitaji kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na elimu ya juu.
Katika hafla ya kutoa zawadi kwa washindi pia wahitimu wa mafunzo ya watendaji katika masoko ya mitaji  nchini walitunukiwa vyeti.
Alisema shindano hilo   awali lilikisiwa kupata washiriki 2000 lakini walipatikana washiriki wapatao 7,791 kutoka vyuo vikuu mbalimbali na elimu ya juu   nchini.
Ofisa Mtendaji Mkuu CMSA,  Nasama   Massinda, alisema mamlaka iliendesha mashindano mawili moja likiwa   la maswali na majibu  na jingine la kuandika insha.
Wavulana sita na wasichana sita wenye alama za juu watagharamiwa safari ya mafunzo nchini Ghana ambako watatembelea Mamlaka ya Usimamizi wa Masoko ya Mitaji,   Soko la Hisa la Ghana na kampuni tano kubwa zinazohusika na utoaji huduma katika masoko ya mitaji.
Dk. Mpango alisema wanafunzi 7,791 walishiriki ikilinganishwa na washiriki wapatao 2,000 waliotarajiwa, hivyo kuvuka lengo la ushiriki kwa asilimia  290.