Na FERDNANDA MBAMILA-DAR ES SALAAM
CHAMA cha Watunisha Misuli Tanzania (TBBF), kimepanga kutoa ajira kwa vijana watakaoshinda kwenye shindano la kutunisha misuli litakalofanyika Desemba 8, mwaka huu.
Katibu Mkuu wa Chama hicho, Francis Mafungilo, alisema lengo la kufanya shindano hili ni kusaidia kuwaondoa vijana katika umaskini na makundi maovu.
Mafungilo alisema mshindi wa kwanza katika shindano hilo atazawadiwa Sh milioni 10, gari, cheti pamoja na medali ya ushiriki, mshindi wa pili atapata Sh milioni 5, cheti na medali ya ushiriki na mshindi wa tatu atapata Sh milioni 2.5, cheti cha ushiriki pamoja na medali ya ushiriki.
Akizungumza kwa niaba ya Kampuni ya Pilipili Entertainment Company Ltd, ambayo ni wadhamini wa shindano hilo, msanii Ahmed Olotu (Mzee Chilo), alisema kampuni hiyo na TBBF imefanya hivyo kwa kuwa imeona umuhimu wa kukuza ajira kwa vijana.