NA RHOBI CHACHA
MWANAMKE ili apate mimba ni lazima awe na sifa za kupata ujauzito na ili mwanamume aweze kumpa mwanamke mimba ni lazima awe na sifa za kumpa mwanamke mimba.
Kama ikitokea mmoja akawa na sifa za kumpa mwenzake mimba na mwingine kupata mimba hapo hakuna tatizom lakini kama mmoja anashindwa kumpa ama mwingine anashindwa kupata mimba hapo kuna tatizo linalohitaji ushauri na uchunguzi wa daktari.
Tatizo hilo lipo kwa wengi, kama lilivyowahi kuripotiwa na baadhi ya wasanii wa fani mbalimbali ambao wanashindwa kupata watoto licha ya kujaribu njia mbalimbali lakini hawakupata mafanikio.
Millen Magese
Miss Tanzania 2001, Happiness/Millen Magese ambaye pia ni mwanamitindo, alionyesha ukomavu na kuwatia moyo wanawake wengi alipoweka wazi kwamba baada ya uchunguzi wa kina na madaktari bingwa wa masuala ya wanawake na uzazi duniani amegundulika kwamba hawezi kupata mimba kutokana na tatizo linalomsumbua la ‘Endometriosis’.
“Tatizo hili huwa linaanzia wakati wa hedhi huwa linanitesa sana tangu nikiwa na umiri wa miaka 13 na limeniathiri hadi leo hii sina uwezo wa kupata mtoto kwa njia ya kawaida. Ila nina nafasi ya kuweza kupata mtoto kwa njia mbadala, mfano kwa njia ya kupandikizwa au kupandikiza kupitia mwanamke mwingine kwa kutumia mayai yangu au njia ya kuasili lakini nimekataa mara kadhaa kubebewa mimba na mwanamke mwezangu,’’ alieleza Magese, alipotembelea Kampuni ya New Habari (2006) Ltd mwaka jana.
Kutokana na tatizo hilo, mwanamitindo huyo amefanya juhudi mbalimbali za kusaidia wanawake wenzake, ikiwemo harakati za kujenga zahanati yenye lengo la kusaidia wanawake wenye tatizo kama lake ambapo wengi wao bado hawajajijua kama wana tatizo hilo.
Wema Sepetu
Mwanamke mwingine aliyeweka wazi kwamba amefanya juhudi mbalimbali kusaka mtoto lakini ameshindwa ingawa hakukata tamaa ni Wema Sepetu, ambaye aliwahi kueleza namna anavyotamani kupata mtoto.
Wema aliwahi kuandika katika kurasa zake katika mitandao ya kijamii kwamba angekuwa na uwezo wa kuzaa angezaa muda mrefu, lakini hana uwezo huo na hawezi kumkufuru Mungu.
“…Au mnadhani siumii mnavyonisema kuhusu kupata mtoto, kumbukeni na mimi ni binadamu, nina moyo kama nyie, au mnadhani napenda kuona wenzangu wakiwa na watoto au ujauzito halafu mimi sina hata wa kusingiziwa… mnadhani nafurahia sio,’’ aliandika kwa masikitiko Wema, akiwalalamikia wanaomsema vibaya kwa kutopata kwake mtoto mapema.
Wasanii wenye matumaini
Wasanii wengine ambao nao licha ya kutokupata watoto kwa muda mrefu lakini wana matumaini makubwa kupata wakati ukifika, wasanii hao ni pamoja na Johari, Koleta Raymond, Amanda, Jacqueline Wolper, Ray C na wengine wengi.
Ray C
Pia muimbaji wa bongo fleva aliyewahi kuwa na majina lukuki likiwemo ‘kiuno bila mfupa’, Rehema Chalamila ‘Ray C’ alisema hamu yake kubwa kwa muda mrefu ilikuwa ni kuwa na mtoto, lakini ameshindwa, licha ya kuwa na uhusiano na wanaume mbalimbali wenye umaarufu.
“Naamini Mungu atanisaidia nitapata motto, bado sijakata tama, lakini hao kina Jide, Wema mi naona kama cha mtoto, mimi tangu nilipovunja ungo, niliwahi kushika mimba mara moja tu nikiwa na Mwisho Mwampamba, lakini bahati mbaya ilitoka, tokea hapo sijapata tena,” alifafanua staa huyo ambaye anadai wapo wenye miaka 45 na wamepata watoto hivyo ipo siku naye atapata.
“Katika miaka 30 natamani sana kuwa na motto, kwani wasichana niliokuwa nao wengi wao wana watoto zaidi ya wawili, hali ambayo inaniumiza sana, pia dawa za kulevya nilizokuwa natumia si sababu ya kutopata motto, kwa kuwa wapo mateja wenye mimba na wengine wana watoto wakubwa,’’ alieleza.
Jacqueline Wolper
“Mimi licha ya kuhangaika muda mrefu bila mtoto bibi yangu ndiye alikuwa mfariji wangu, kwani nilipofika Moshi cha kwanza aliniuliza kuhusu motto, kiukweli nilitokwa na machozi, alitonesha kidonda changu,’’ anaeleza Jacqueline namna anavyosikitishwa na kutopata mtoto mapema.
Wolper alisema amejitahidi sana kutafuta mtoto lakini imeshindikana.
“Nimejitahidi sana kusaka mtoto lakini imeshindikana, hivyo kwa wale ambao wanabahatika kupata mimba nawashauri wasitoe maana mtoto ni faraja kubwa kwa wanawake,” alieleza.
Lady Jaydee
Mwanamuziki huyo naye aliwahi kudaiwa kutokuwa na uwezo wa kupata mtoto kutokana na kuwa muda mrefu katika mahusiano lakini hana mtoto.
Pia iliwahi kuelezwa kwamba alijaribu kufanya njia mbalimbali za kupata motto, lakini bado hajafanikiwa kumpata mtoto ingawa anaendelea kumuomba Mungu ili aweze kupata mtoto.
Johari
Mwigizaji huyu wa filamu, Blandina Chagula ‘Johari’ amedai kwamba licha ya kutopata mtoto kwa muda mrefu, lakini imani yake ni kwamba kizazi chake kinafanya kazi na kinasubiri mwanamume wa kumuoa ili wafanikishe kupata mtoto badala ya kupata mtoto nje ya ndoa.
“Kizazi changu kinafanya kazi, ingawa nina umri mkubwa sijapata mtoto lakini sitaki kupata mtoto kabla ya kuolewa, siwezi kufanya jambo kwa kufurahiasha watu hadi nitakapopata mume bora,” alifafanua Johari.
Koleta Raymond
“Mimi siangalii ndoa, naangalia mtoto, siku yoyote nikipata mimba nitaitunza nizae, kwa kuwa nataka mtoto wakati wowote, ndoa itakuja baadaye kama nitajaaliwa kuolewa, ila ndoto na tamaa yangu ni kupata mtoto,’’ alieleza Koleta.
Amanda
“Mimi nimekaa muda mrefu bila kupata mtoto, mimeolewa na kuachika bila kupata mtoto, hapa nina woga wa kwamba nina tatizo la kupata mtoto, nina wasiwasi na kizazi changu ingawa namuamini Mungu, akipenda kufanya yake nitampata huyo mtoto licha ya kumtafuta muda mrefu kwa juhudi kubwa,’’ alieleza Amanda, huku akidai kwa sasa upendo wake ameuweka kwa paka anayemfuga nyumbani kwake kama mtoto wake mbadala.
Baby Joseph Madaha
Mwanamuziki na mwigizaji huyu naye ameweka wazi kwamba licha ya kutamani kuwa na motto, bado hajamuona mwanamume wa kuzaa naye.
“Japo napenda kuwa na mtoto ila sijampata mwenye sifa za kuwa baba watoto wangu ili watoto wajivunie baba yao na wawe na maisha mazuri,’’ alisema Baby Madaha.
Mayasa Mrisho
Mwigizaji mwingine anayetufungia makala yetu hii ni Mayasa Mrisho, ambaye amedai licha ya kujitahidi kuwa na wanaume tofauti kimapenzi, lakini hakuwahi kufanikiwa kupata mtoto.
“Kiukweli nimekuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanaume wengi lakini sikuwahi kupata motto, naumia sana, umri unaenda na rafiki zangu wengi wana watoto,’’ alieleza kwa masikitiko Maya.