Derick Milton, Simiyu
Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) la Sabasaba wilayani Tarime mkoani Mara, limetangaza siku 100 za maombi kwa ajili ya kuliombea taifa na dunia kwa ujumla kutokana na kukumbwa na ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona.
Maombi hayo yatahusisha waumini wote wa kanisa hilo, ambapo watalazimika kufunga kwa siku hizo huku wakimuomba Mungu kutokomeza janga hilo ambalo limesababisha maelfu ya vifo vya watu duniani.
Mchungaji wa kanisa hilo, Adili Ndimangwa amesema wamefika uamuzi huo kutokana na ugonjwa huo kuendelea kuwa tishio kubwa la dunia ikiwamo Tanzania.
Amesema kama kanisa wanao wajibu wa kuisaidia dunia na Watanzania kwa ujumla katika mapambano ya ugonjwa huo, ambao bado hajapata dawa wala kinga.
Amesema mbali na kufuata ushauri wa watalaamu wa afya jamii lazima irudi kwa Mungu ambaye ndiye mwenye uwezo wa kupambana na janga hilo lililowashinda binadamu.
“Kama Kanisa tumetangaza siku 100 za maombi waumini wa kanisa hili wataomba siku tatu ndani ya wiki moja, hadi tufikishe ziku zote 100, hatuwezi kuwaachia tu watalaamu kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa huu,” amesema Mchungaji Ndimangwa.