NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WAPINZANI wa Yanga katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika, Cercle de Joachim ya Mauritius, wamezidi kuwa na hali mbaya kuelekea pambano lao la Februari 13 mwaka huu kutokana na kupata matokeo yasiyoridhisha katika Ligi Kuu ya nchini Mauritius.
Mabingwa hao wa Mauritius msimu uliopita walishika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi wakiwa wamejikusanyia pointi 24 baada ya kushuka dimbani mara 15 na kushinda mechi 7, kupata sare mara tatu na kufungwa mara tano.
Katika mechi sita walizocheza mfululizo, Cercle de Joachim wamefanikiwa kushinda dhidi ya Pamplemousses na Curepipe Starlight ikapata sare mbili dhidi ya Grande Rivier na Chamarel pamoja na kufungwa na Petite Rivier na La Cure Sylvester.
Matokeo hayo ya Cercle de Joachim yana tofauti kubwa na wapinzani wao Yanga ambao wameshuka dimbani mara 15 na hawajafungwa mchezo hata mmoja, huku wakiwa wanaongoza kwenye msimamo wa ligi kwa kufikisha pointi 39.
Katika mechi sita ambazo Yanga wamecheza mfululizo, wamefanikiwa kuibuka na ushindi mara tano na kupata sare moja hali inayowaongezea sifa ya ubora kwa kuwazidi wapinzani wao kila idara kutokana na michuano wanayoshiriki kwenye nchi zao.
Katika mechi hizo sita, Wanajangwani hao wameshinda mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar, wametoka sare ya kutofungana na Mgambo Shooting, wameifunga Stand United 4-1, wameichapa Mbeya City 3-0, wameibuka na ushindi wa 1-0 kwa Ndanda FC kabla ya kuiadhibu Majimaji FC kwa mabao 5-0.
Yanga wamecheza mechi 15 za ligi sawa na Cercle de Joachim, lakini wawakilishi hao wa Tanzania wamefanikiwa kuvuna jumla ya pointi 39 tofauti na wapinzani wao wenye pointi 24, hivyo kwenye Klabu Bingwa Afrika Wanajangwani hao wanaweza kutumia fursa hiyo kuwaondosha mapema katika michuano hiyo.
Kutokana na michezo 15 waliyocheza Cercle de Joachim, wamepachika wavuni mabao 21 na kuruhusu nyavu zao kutikisika mara 17 wakati Yanga wamefunga mabao 36 huku wakikubali kufungwa mabao matano tu na kuwa timu pekee iliyofungwa mabao machache hadi sasa katika Ligi Kuu Bara.
Februari 13, mwaka huu Yanga itaanza kampeni zake kwenye Klabu Bingwa Afrika ikiwa ugenini na timu hizo zinatarajiwa kurudiana Februari 26, mwaka huu jijini Dar es Salaam.