Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Wenyeviti wa mashina katika Kata ya Liwiti Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wametakiwa kuwasajili wageni na wapangaji wote katika daftari la wakazi ili kudhibiti vitendo vya uhalifu.
Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye ofisi za Serikali ya Mtaa Liwiti, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Liwiti, Ignas Maembe, amesema kwa kutambua umuhimu wa wenyeviti wa mashina wameandaa waraka ambao unalenga kusimamia ulinzi na usalama katika ngazi ya kaya na mtaa.
Amesema kila mwenyekiti wa shina anatakiwa kuhakikisha kwamba wanawatambua wakazi pamoja na kuwabaini wapangaji wapya wanaohamia na kuhamasisha wananchi kushiriki na kuchangia gharama za ulinzi kulingana na taratibu za mtaa husika.
“Kila mtaa unatakiwa kuwa na rejista ya wakazi wake ili kufahamu kwa ukamilifu idadi ya watu kwenye kila kaya. Kila mjumbe ahakikishe anawasomea wamiliki na wapangaji wa nyumba waraka huu ili waweze kuelewa vizuri,” amesema Maembe.
Kuhusu suala la usafi wa mazingira amesema wanaendelea kusimamia wananchi kwa kuhakikisha kila kaya inalipia ada ya uzoaji taka pamoja na kufanya usafi kwenye maeneo yanayowazunguka kama sehemu za biashara, nyumba za kuishi, mifereji, gereji na baa.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Liwiti, Arafa Mshana, amesema wanahimiza ulinzi shirikishi na kwamba wamewaelekeza wajumbe wa mashina yote ya mtaa huo kuhakikisha vijana wa ulinzi shirikishi wanapatikana waweze kupatiwa mafunzo ambayo yanatolewa kila Jumapili katika kituo cha polisi Tabata.
Kwa upande wake Mkuu wa Kituo cha Polisi Tabata, Mrakibu wa Polisi Colle Senkondo, amewataka wananchi kutoficha wahalifu na kuonya kuwa wale wote wanaokwamisha ulinzi na usalama watashughulikiwa.
“Unapomtambulisha mpangaji wako inakusaidia pia wewe huenda kuna rekodi zake ziko kwa mwenyekiti. Watu wamekuwa hawana amani wanakwapuliwa simu, wanavunjiwa majumba yao.
“Sisi peke yetu hatuwezi ndiyo sababu mnaona tunaendeleza mafunzo ya ulinzi shirikishi tunawapa mafunzo tukifahamu wao ni mkono wetu wa pili,” amesema Senkondo.
Mmoja wa wajumbe wa Shina namba 6 Misewe B, Anthony Lyimo, amesema watatoa ushirikiano ili kukomesha vitendo vya uhalifu katika maeneo yao.