23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Samia aagiza Wizara ya madini kuitangaza Tanzanite

Sheila Katikula na Clara Matimo-Mwanza

Rais Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Madini kuhakikisha inasimamia vizuri uzalishaji na uuzaji wa madini ya Tanzanite ili yaweze kuinufaisha nchi na kuitangaza kimataifa kwani ni rasilimaliinayozalishwa na Tanzania pekee duniani.

 Rais Samia Suluhu akiweka jiwe la Msingi katika kiwanda cha kusafisha dhahabu Mwanza Precious Metal Refinery kilichopo wilaya ya Ilemela mkoani hapa. Picha Na Ikulu Mawasiliano.

Rais Samia ameyasema hayo leo Jumamosi Juni 13, 2021 wakati akizungumza na wadau wa sekta ya madini, viongozi mbalimbali na wananchi baada ya kuzindua kiwanda cha kusafisha dhahabu Mwanza Precious Metal Refinery kilichopo wilaya ya Ilemela mkoani hapa kilichojengwa kwa thamani ya Sh bilioni 12.2.

Amesisitiza kwamba madini hayo yanayochimbwa mkoani Manyara yanatakiwa kupewa uthamani wa kipekee kwani ndiyo utambulisho wa Tanzania katika sekta ya madini duniani ili taifa na wananchi wake waweze kunufaika na uwepo wa rasilmali mali hiyo.

“Mwenyezi Mungu ametupendelea sana watanzania akatupatia rasilimali ambayo tunayo pekee yetu dunia nzima hivyo ni wajibu wetu kuilinda ili itufaishe na tuone uthamani wake.

“Tusipokuwa makini haitatunufaisha maana Sasa ni kama madini haya yanachimbwa nchi nyingi dunia maana ukienda kwenye nchi za jirani utakuta kuna Tanzanite nyingi  hata Kule bara la Asia utaikuta  na hata dunia kote sasa inapatikana hivyo inatakiwa kuanzisha mchakato wa kuhakikisha tunakuwa na nembo maalum ambayo itaitambulisha rasilimali hiyo,” amesema Rais Samia.

Amesema madini ni rasilmali ambayo siku moja itakwisha ikiwemo Tanzanite hivyo inapaswa kuwekewa mfumo bora ambao utakuwa na tija kwa taifa.

“Nakuagiza Waziri wa madini kaa na wawekezaji katika sekta hii ili wapendekeze mfumo mzuri utakao yalinda madini haya adhimu ya Tanzanite pia endelea kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo ili waweze kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa,wao binafsi pamajo na familia zao pia wasaidie upatikanaji wa malighafi itakayotumika kiwandani hapa,” amesema Rais Samia.

Naye Waziri wa Madini, Dotto Biteko amesema kiwanda hicho cha kusafisha dhahabu kinauwezo wa kuzalisha kilo 480 kwa siku kutokana na upatikanaji wa malighafi kwa sasa.

“Lakini kiwanda hiki kinauwezo wa kusafisha kilo 960 kwa siku endapo malighafi ikipatikana, mtambo wa kusafisha dhahabu uliofungwa unakiwango cha kimataifa unawezesha dhahabu kusafishwa kwa alisimila 99.9 hivyo uwepo wake umeiingiza nchi yetu kwenye medani za wasafisha dhahabu  duniani,”amesema Biteko.

Naye Mkurugenzi wa kiwanda cha Mwanza Precious Metal Refinery, Anand Mohan Mahajan, amesema kiwanda hicho kinanunua na kusafisha madini hivyo anaiomba Serikali iwasaidie kuzuia usafirishwaji wa dhahabu ambayo ni malighafi kwenda nje ya nchi ili dhahabu yote ipatiwe  thamani ndani ya nchi.

Mahajan alisema  wametenga jumla ya Sh bilioni 346.5 kwa ajili ya kununua malighafi hivyo wachimbaji na wafanyabiashara wasiwe na wasiwasi kwa sababu kuna soko la uhakika.

Ujenzi wa  kiwanda hicho ulianza machi 15 mwaka jana na umekamilika machi mwaka huu na kukamilika kwake kutakuwa na faida mbalimbali kwa taifa ikiwemo utoaji wa ajira.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles