Waziri wa Maliasi na Utalii, Dk. Khamis Kigwangala amesema Serikali inakusudia kuanzisha mitihani ya kitaifa kwa waongoza watalii (Tour Guide) wote ili kuimarisha sekta hiyo nchini.
Dk. Kigwangala amesema hayo leo mchana wakati akizungumza na wafanyakazi wa Shirika la Hifadhi za Taifa nchini (TANAPA) mjini Arusha.
Amesema kusudio hilo linalenga kuimarisha zaidi sekta ya utalii hususani kwa waongoza watalii ambao aliwataja kama mlango ambapo wakiwa na lugha mbaya, vitendo vya udokozi kwa wageni serikali haiwezi kuwa na sifa nzuri kwa wageni ambao ni mabalozi wa Tanzania nje.
“Kumekuwa na malalamiko mengi katika eneo hili, wageni wamelalamika sana. Kama tutakuwa na huduma nzuri katika eneo hili basi tutakuwa tumetengeneza soko zuri kwa mabalozi wanaotutembelea,” amesema Dk. Kigwangala.
Pia amesema kusudio hilo la kufanya mitihani litakwenda sanjari na utoaji wa vyeti ambavyo vinatambulika na wizara ambapo kila muongoza watalii atalazimika kuwa nacho ili aweze kufanya kazi hiyo hatua ambayo itasaidia kuondoa vitendo vya sekta ya utalii kuchafuliwa na watu wasio na maadili.