ELIZABETH KILINDI-NJOMBE
WATU wanne wamefariki dunia kwa kupigwa na radi akiwemo mwanafunzi wa darasa la saba wa Shule ya Msingi Mtapa wilayani Wanging’ombe, Haridi Hamisi (13), aliyekuwa akitoka kwenye mitihani ya kujipima huku wawili wakijeruhiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Salum Hamduni, alisema matukio hayo yametokea Machi 28, mwaka huu katika maeneo mbalimbali mkoani hapa.
Alisema katika tukio la kwanza lililotokea saa 10 jioni katika Kijiji cha Igwachanya wilayani Wanging’ombe, ambapo mwanafunzi Haridi alipigwa na radi na kufariki dunia alipokuwa akitoka Kijiji cha Dulamu katika mitihani ya kujipima ya kata.
“Wakati tukio hili linatokea, alikuwa akirejea nyumbani akiwa anaendesha baskeli yake, kwa bahati mbaya alipigwa na radi na kusababisha mauti yake,” alisema Kamanda Hamduni.
Alisema tukio jingine ni Yohana Mayala mkazi wa Kijiji cha Idunda akiwa na familia yake ya watu wawili ndani nyumba, walipigwa na radi na kusababisha kifo chake huku mama yake Imani Mayala na Scholastica Elia (13) ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya msingi Idunda wakijeruhiwa.
“Wote kwa pamoja walipatiwa matibabu ya awali katika Zahanati ya Idunda na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa Kibena kwa matibabu zaidi,” alisema.
Alisema tukio jingine lilitokea katika Kijiji cha Miva, Kata ya Luponde wilayani Njombe, ambapo Godfrey Ogini (35) na Telius Geogre (30) wakiwa nyumbani, walipigwa na radi na kufariki dunia.