Na Mwandishi Wetu, Njombe
Watu wanne akiwemo Mkuu wa Chuo cha Uuguzi Lugarawa, Steven Mtega(39) wamefariki dunia kwa kuzama kwenye mto Lupali wakiwa kwenye gari waliyokua wakisafiria kata Lugarawa wilayani Ludewa mkoani Njombe.
Akizungumza na www.mtanzania.co.tz kwa njia ya simu Mganga Mkuu wa wilaya ya Ludewa Dk. Stanley Mlay, alisema tukio hilo limetokea Febuari 27, usiku ambapo marehemu hao walikua kwenye gari aina ya Harrier ambapo walikua Lugarawa kwenye mapumziko.
“Walipata ajali kwenye mto Lupali huu mto sasa hivi una maji mengi kwa sababu ya mvua zinavyonyesha walikua watu wanne kwenye mambo yao ya mapumziko Lugarawa na dereva alikua huyo mkuu wa chuo wakasema wabadilishe maeneo waende Mundindi sasa walivyofika maeneo hayo ndo wanaingia mtoni,” alisema Mlay.
Mlay aliwataja marehemu wengine kuwa Marko Mpete, Fundi umeme wa Lugarawa Merk Mwalongo(35) Mjasiriamali Rukia Mfaume(28) alikuwa Mhasibu wa Mradi wa umeme wa Akra Lugarawa
Hata hivyo alisema miili hiyo iko chumba cha kuhifadhia maiti Hospital ya Lugarawa ikisubiri taratibu za mazishi kukamilishwa.
Naye Diwani wa kata ya Lugarawa, Erasto Mhagama, akizungumza kutokea kwa tukio hilo alisema tukio hilo limetokea mpakani kwa kijiji cha shaurimoyo na kijiji cha amani.