Na MOHAMED HAMAD-KITETO
LUGHA za kejeli, matusi na vipigo kwa wajawazito wilayani Kiteto mkoani Manyara, vimetajwa kuwa sababu za wanawake kutaka kufunga uzazi ili kujiepusha na adha hizo.
Akizungumza mbele ya Mbunge wa Kiteto, Emmanuel Papian (CCM), mmoja wa wanawake hao, Farida Omari, alisema wamekuwa wakilalamikia kauli na vitisho vya wauguzi hospitalini bila kupatiwa ufumbuzi hivyo wanaona suluhisho pekee ni kufunga uzazi.
Alisema mbali na matusi, kejeli, vipigo wakati wa kujifungua, baadhi yao wamekuwa wakitelekezwa kwa kunyimwa msaada wakati wa kujifungua na huachwa peke yao bila usaidizi wowote wakiambiwa hakuna mipira ya kuvaa mkononi (gloves).
“Mama mjamzito akienda Hospitali ya Kiteto mambo anayokutana nayo ni makubwa utadhani yuko kwenye mapambano na FFU, hili
halivumiliki mheshimiwa mbunge tunaomba kero hii iishe kwani kuendelea kwake kutaleta madhara makubwa,” alisema Farida.
Akijibu ombo hilo, Mbunge huyo alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kuchukua hatua dhidi ya watumishi wa aina hiyo ambao hawatumikii nafasi zao ipasavyo.
“ Ndugu yangu Kambona (mkurugenzi) unataka ushahidi gani? hili halitoshi kuchukua hatua? Nakumbuka haya malalamiko ni ya muda mrefu sana kwani yamekuwa yakijirudia katika hospitali hii. Amka sasa timiza wajibu wako kwani kutofanya hivyo ni hatari ambayo itatugharimu baadaye,” alisema Papian.
Alisema kama mwakilishi wa wananchi hatakuwa tayari kuona wananchi wakinyanyasika wanapohitaji huduma za jamii, huku akisisitiza kuwa mtumishi wa umma asiyeendana na kasi ya Rais Dk. John Magufuli hatavumiliwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kiteto, Tamimu Kambona, aliwataka wanawake hao kuendelea na uzazi huku akisema, ameshamwandikia barua ya kumshusha cheo Muuguzi mkuu, Dk. Samsom Nyakibali ambaye ameshindwa kuitendea haki nafasi yake.