26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

WANAWAKE WANAHATARI YA KUVUNJIKA MIFUPA KULIKO WANAUME

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

WATU zaidi ya 10 kila wiki wanapokewa na kulazwa wodini katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Mishipa ya Fahamu, Mgongo, Ubongo na Uti wa Mgongo Muhimbili (MOI), kutibiwa tatizo la kuvunjika mifupa.

Kati ya watu hao wanawake hasa wenye umri wa miaka kuanzia 50 na kuendelea ndiyo ambao huwa wengi zaidi kuliko wanaume na watoto.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi katika mahojiano maalum yaliyofanyika ofisini kwake hivi karibuni, Daktari Bingwa wa Mifupa MOI, Joseph Mwanga alisema tatizo hilo kitaalamu huitwa Pathological fracture.

“Tatizo hilo hutokea kwa kutumia nguvu kidogo tu, kisababishi kikubwa ni mfupa kupungua nguvu yake na uwezo wa kushikilia mwili na kuzuia ukinzani (force) wowote unaoweza kutokea.

“Yaani ule mfupa unapoteza ile nguvu (capacity) na kuwa teketeke (mlaini) hali inayosababisha kushindwa kuzuia ukinzani wowote ule unapotokea,” alifafanua.

Daktari huyo aliongeza “Kwa kawaida mfupa umeundwa ukiwa na sehemu mbili, ya ndani na nje, ile ya ndani huwa ina uteute (bone marrow) na uimara wa mfupa hutokana na kile kipenyo chake ambacho huwa na ule uteute.

“Kile kipenyo kikizidi kuongezeka maana yake ile sehemu ya nje ya mfupa inapungua ubora wake,” alisema.

Wagonjwa

Akisimulia jinsi alivyopata tatizo hilo, Rosemary Msumeno (75), Mkazi wa Kilimanjaro, alisema amevunjika mguu wake wa kulia baada ya kuanguka ndani nyumbani kwa mwanawe (hapa Dar es Salaam).

“Ilikuwa usiku wa saa tano, nakumbuka tulipomaliza kusali nilimwambia mjukuu wangu tumwage maji ya baraka ndani sasa nilipita nikiwa nimebeba ndoo kumbe chini kulikuwa na maji na nyumba ile ina tarazo nikaanguka na kuvunjika,” alisema.

Naye, Kolabita Israel (67), Mkazi wa Njombe alisema alianguka nje ya nyumba yake na kuvunjika mguu wa kushoto na nyonga.

“Nimepimwa nikaambiwa pressure yangu ipo juu unabidi nisubiri ishuke ndipo nifanyiwe upasuaji,” alisema.

Naye, Rosemary Mtimizi (74), Mkazi wa Magomeni alisema alianguka akiwa anashuka kwenye ngazi ofisini kwake.

“Palikuwa pakavu kabisa na nilikuwa nimevaa viatu vya chini lakini nilishangaa tu nilipoteleza nilipotaka kuinuka sikuweza na nilihisi maumivu makali na mguu ulikuwa umevimba,” alisema.

Kwanini wanawake

Alisema umri unaposonga mbele kwa wanawake hasa kuanzia miaka 45 na kuendelea kibaiolojia hukoma kupata mzunguko wa kila mwezi (hedhi) kitaalamu hali hiyo inaitwa osteoporosis.

“Ni kipindi cha ‘menopause’ anapokuwa katika hali hiyo hupelekea mwili wake kuwa na uwiano duni (in-balance) wa vichocheo (hormone) ya estrogen na progesterone.

“Kimsingi vichocheo hivyo ndivyo ambavyo husaidia kujenga mfupa na ndivyo ambazo husababisha calcium kufyonzwa na kutengeneza mfupa.

“Sasa zinapokuwa in-balance maana yake ni kwamba ile calcium hupotea na mifupa huanza kuwa teketeke,” alibainisha.

Alisema sababu nyingine inayosababisha mifupa kuwa teketeke ni kitendo cha mtu kulala muda mrefu kitandani na kutoufanyisha mwili wake shughuli mbalimbali ikiwamo mazoezi.

“Kitendo cha kutokuitumia mifupa hupelekea kuwa teketeke, kwa kawaida mifupa ili ijijenge lazima ifanyishwe kazi lakini isipofanyishwa kazi huwa haijijengi.

“Aidha, mgonjwa aliyepata tatizo la kuvunjika kwa mfano uti wa mgongo au aliyepooza mwili mara nyingi mifupa yao huwa teketeke,” alisema.

Alisema tatizo hilo huwa haliwapati zaidi wanaume kama ilivyo kwa wanawake kwa sababu homoni ya estrojeni wanayo wanawake.

“Vile vile hawapati tatizo hili zaidi kama wanawake kutokana na zile shughuli zao za kila siku wanazofanya mara kwa mara ambazo hufanya mifupa yao kuwa imara,” alisema.

Aliongeza “Wanawake wengi wanapofikia umri wa kukoma hedhi hupata uzito mkubwa na kuwafanya washindwe kutembea na wengi hukaa nyumbani hali hiyo husababisha mifupa yao kuwa teketeke.

Kuhusu watoto

Dk. Alisema kwa upande wa watoto nao hupata tatizo hilo hata hivyo huwa ni mara chache mno kulinganisha na watu wazima.

“Ikitokea mtoto amepata tatizo hili huwa kuna mambo mengi, kwa mfano ikiwa mwili wake utashindwa kutengeneza calcium au ikiwa atapata maambukizi ya mifupa ama jipu la mfupa huweza kusababisha kuvunjika mifupa yake,” alibainisha.

Alisema wagonjwa wa saratani ya mifupa nao huwa kwenye hatari ya kupata tatizo hilo.

Matibabu

Alisema kwa kawaida matibabu yake huwa ni upasuaji hata hivyo huwa magumu zaidi kwa upande wa watu wazima kuliko watoto.

“Kwa upande wa watu wazima huwa magumu kwani mifupa ile hupoteza nguvu yake huwa tunaweza vyuma lakini kuna uwezekano mkubwa wa kushindwa kushika kama inavyotarajiwa.

“Miongoni mwao huja wakiwa na magonjwa mengine kwa mfano moyo, kisukari, shinikizo la damu na wapo ambao kiwango cha utendaji kazi wa moyo wao huwa ni chini ya asilimia 50.

“Hivyo unakuta haiwezekani kumpatia dawa ya usingizi ili kumfanyia upasuaji tunachofanya tunawasaidia kuvuta mguu kwa kutumia vifaa tulivyonavyo nay ale maumivu upungua taratibu na baadae tunamruhusu kurejea nyumbani ambako hulazimika kutembea na magongo,” alisema.

Aliongeza “Lakini kama mgonjwa yupo ‘fi’t tunaweza kumfanyia upasuaji ikiwamo kumuwekea viungo vya bandia.

“Kwa watoto kama mifupa imeoza tunakata kipande kilichooza, palipovunjika tunarekebisha na tunanyoosha mfupa kwani bila kufanya hivyo mfupa ule unaweza kuwa mfupi lakini kama imeoza sana tunalazimika kukata kiungo husika.

“Kwa sababu kama ana jipu la mfupa, mnaweza kumtibu hata miaka mitano usaha unakuwa unarudi mara kwa mara na unaweza kumsababishia kupata maambukizi na hata kutoka damu,” alisema.

Kinga

Daktari huyo alishauri jamii kuzingatia kuwawahisha hospitalini watu wenye matatizo ya namna hiyo ili wakapate tiba stahiki mapema.

“Wasikimbilie kwa waganga wa kienyeji, wengi huja wakiwa wamechelewa hasa wa saratani huja ikiwa tayari imesambaa na hivyo kufanya matibabu yao kuwa magumu,” alisema.

Alishauri kula mlo kamili uliojumuisha makundi yote matano ya vyakula ili kupata lishe inayohitajika mwilini pamoja na kufanya mazoezi.

“Kwa wakina mama wale ambao wamefikia ukomo wa hedhi waje hospitalini tutawasaidia kuwapatia dawa maalum ambazo zipo zenye uwezo wa kuimarisha mifupa ya mwili.

“Lakini pia jamii inapaswa kuwa makini pale wanapoamua kuweka tarazo ndani ya nyumba zao kwani wapo ambao huteleza ndani na kuvunjika,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles