HADIA KHAMIS NA YASSIN ISSAH, DAR ES SALAAM
MKOA wa Kagera unaongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha kina mama wasionyonyesha watoto wa umri wa chini ya miezi sita, hali inayosababisha udumavu wa akili kwa watoto hao, imeelezwa.
Hali hiyo pia inaufanya mkoa huo uongozwa kwa vifo vingi vya watoto wenye udumavu na wa umri chini ya miaka mitano.
kwa zaidi ya asilimia 40,kutokana na kukosa kunyonya ipasavyo imeelezwa.
Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania(TFNC) umeitaja mikoa mingine yenye kiwango kikubwa cha kina mama kutonyonyesha kuwa ni Iringa, Njombe, Ruvuma, Rukwa, Kigoma, Katavi na Geita.
Takwimu hizo zilitolewa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Uzazi na Afya ya Mtoto katika Wizara Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dk. Georgina Msemo, Dar es Salaam jana.
Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari katika uzinduzi wa Wiki ya Unyonyeshaji.
Dk. Msemo alisema maadhimisho ya Siku ya Unyonyeshaji mwaka huu yatafanyika mkoani Kagera.
Alisema unyonyeshaji maziwa ya mama pekee kwa mtoto chini ya miezi sita unasaidia kukuza akili ya mtoto na kupunguza magonjwa yasiyokuwa ya lazima.
Kulisha mtoto chini ya miezi sita vyakula vya nyongeza bado ni tatizo nchini.
Alisema takwimu zinaonyesha asilimia tano ya watoto chini ya miezi sita wanapewa chakula au vinywaji kwa kutumia chupa.
Dk. Msemo alisema utafiti unaonyesha asilimia 32 na 24 ya watoto wanaozaliwa vijijini na mijini hupewa kinywaji au chakula kingine hata kabla ya kuanzishiwa maziwa ya mama.
“Utafiti huo unaonyesha kuwa ni asilimia 50 tu ya watoto wa umri wa mwezi 0 mpaka sita hunyonyeshwa maziwa ya mama pekee.
“Wakati huo huo takwimu zinaonyesha asilimia 81 ya watoto wa miezi miwili hunyonyeshwa maziwa ya mama pekee,” alisema.
Alisema idadi ya watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee huendelea kupungua kadri umri unavyoongezeka.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa TFNC, Dk.Sabas Kimboka, alisema Tanzania imefanya juhudi kubwa kuboresha ulishaji wa watoto wachanga na wadogo, lakini hali bado hairidhishi.
Alisema asilimia 97 ya wanawake nchini hunyonyesha watoto wao, lakini unyonyeshaji huo haufuatwi ipasavyo.
“Utafiti wa hali ya demografia na afya nchini mwaka 2010, unaonyesha unyonyeshaji wa maziwa ya mama ndani ya saa moja ya kwanza baada ya kujifungua ni asilimia 49 ikilinganisha na asilimia 59 ya mwaka 2005.
“Hali hii huchangiwa kwa kiasi kikubwa na idadi ndogo ya wanawake wanaojifungulia katika vituo vya afya ambao ni asilimia 50,”alisema Dk.Kimboka.
Alisema utafiti mbalimbali unaonyesha asilimia 58 ya wanawake waliojifungua kwa usaidizi wa wauguzi wenye elimu na ujuzi, wana uwezekano mkubwa wa kuwanyonyesha watoto wao ndani ya saa moja, kuliko waliozalishwa na wakunga wa jadi.