Na Shomari Binda, Butiama
Wanawake wilayani Butiama mkoani Mara wametakiwa kutumia simu janja walizopewa (Smartphone) kutoa taarifa za ukatili kwenye maeneo yao ili kuisaidia Serikali na wadau kukomesha matukio hayo.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Butiama, Josiah Peter, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya namna ya kutoa taarifa kutumia simu janja (Smartphone).
Amesema taarifa nu kitu muhimu katika kukabiliana na masuala ya ukatili na kuwataka wanawake wanaoshiriki mafunzo hayo kuwa mabalozi wazuri.
Peter amesema yapo matukio ambayo yanatokea kwenye jamii ya ukatili ambayo hayatolewi taarifa na kupelekea kuendelea kukithiri kwa matukio hayo.
“Nilishukuru sana Shirika la Hope for Girls and Women kwa mafunzo haya ambayo yatawawezesha wanawake kutoa taarifa za matukio ya ukatili. Naamini Wanawake hawa wakitoka hapa watakwenda kuwa mabalozi wazuri na watatusaidia sisi kama serikali pamoja na wadau kuweza kutekeleza majukumu yetu,”amesema Petere.
Mkurugenzi wa Shirika hilo, Rhobi Samweli, amesema mafunzo hayo yatawashirikisha wanawake 59 kutoka vijiji vya Butiama lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa kutoa taarifa za ukatili.
Amesema licha ya kutoa mafunzo lakini wanawake hao watakabidhiwa simu janja kila mmoja kwa ajili ya utoaji wa taarifa hizo na kulishukuru shirika la UNFPA kwa kutoa simu 310 zenye thamani ya Sh milioni 21.
Baadhi ya wanufaika wa mpango huo wameshukuru kupata mafunzo ambayo yatawasaidia kutoa taarifa za ukatili.