Christina Gauluhanga – Dar es Salaam
NGOME ya Wanawake ya Chama cha ACT Wazalendo, imetangaza kikosi kazi ambacho kitarahisisha ushindi katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa ngome hiyo Taifa, Mkiwa Kimwanga alisema uteuzi huo wa makatibu na manaibu wao sasa unakwenda kuimarisha safu ya ushindi kupitia wanawake katika uchaguzi wa rais, wabunge, madiwani pamoja na urais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Alisema uteuzi wa majina hayo umezingatia vigezo na wateule hao wa kamati mbalimbali watatumikia katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
“Lengo la ngome yetu ni kuongeza idadi ya wapigakura na kushika nafasi ya urais na hata ubunge kwa Tanzania Bara na Visiwani kwani tunaamini wapigakura wengi ni wanawake na kwa mwaka huu tumejipanga vema,” alisema Mkiwa.
Alitaja kamati hizo na viongozi wake kuwa ni pamoja na Itikadi, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma ambayo Katibu ni Raya Ibrahim Khamis na Naibu Katibu ni Ashura Ali.
Kamati ya Mipango na Uchaguzi, Katibu ni Mary Boniphace na Naibu Katibu ni Lutfiya Kassim Juma na Kamati ya Uadilifu, Katibu wake ni Fuata Mussa Mbaraka na Naibu Katibu ni Rabia Omary Kaliji.
Kamati nyingine ni ya Fedha, Miradi na Uchumi, Katibu wake ni Khadija Salum Ali na Naibu Katibu ni Chiku Aflah Abwao na Kamati ya Jinsia Wanawake Wenye Mahitaji Maalumu, Katibu ni Raisa Abdallah Mussa na Naibu wake ni Bahati Hamad Chirwa.
Alisema baada ya uteuzi huo wateule hao watakutana nao kwa lengo la kupangiana majukumu na kuimarisha chama upande wa Tanzania Bara na Visiwani.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ngome hiyo, Elizabeth Magwaja, alisema kuwa wana imani na safu hiyo kwa kuwa ni wazoefu katika shughuli za kisiasa.
Alisema lengo na tegemeo kuu la ngome hiyo ni kuhakikisha wanaibuka na ushindi wa kishindo na kuongeza idadi ya wanawake viongozi hapa nchini.